ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 11, 2017

LHRC YAWANOA VIONGOZI WA DINI KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA

 Mkurugenzi wa Baraza la Dini na Amani Tanzania (IRCPT), Mchungaji Thomas Godda, akihutubia wakati akifungua semina ya siku mbili ya viongozi wa dini kuhamasisha uhiishaji wa katiba mpya inayoendelea Hoteli ya Golden Tulip Posta jijini Dar es Salaam leo. Semina hiyo imeandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
 Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumza kuhusu umuhimu wa semina hiyo kwa viongozi wa dini.
 Meneja Mipango Msaidizi wa (IRCPT), Rogers Fungo akizungumza katika semina hiyo.

Mwenyekiti wa Taifa wa Wanawake wa Baraza la Kiislam Tanzania (Bakwata), Shamim Khan (kulia), akizungumza katika semina ya siku mbili ya viongozi wa dini kuhamasisha uhiishaji wa Katiba mpya iliyofanyika Dar es Salaam leo. Semina hiyo imeandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
 Semina ikiendelea.
 Wapiga picha wakichukua tukio hilo.
 Wawakilishi kutoka taasisi za dini wakiwa kwenye semina.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye semina.

Na Dotto Mwaibale

BARAZA la Uongozi la Dini na Amani Tanzania  (IRCPT), limesema ipo haja mchakato wa Katiba Inayopendekezwa kufikia tamati kwa kuwa ina mambo ya msingi kwa Watanzania.

Mkurugenzi wa Baraza hilo, Mchungaji Thomas  Godda amesema ni vema viongozi wa dini  wakatimiza wajibu wao  kwa kuihamasisha  Serikali imalize mchakato huo sanjari na kuhamasisha wananchi kusoma Katiba iliyopo ili kuwajengea uelewa mpana.

Ametoa kauli hiyo leo Dar es Salaam kwenye semina ya siku mbili ya kuhamasisha uhiishaji wa Katiba Mpya kwa viongozi wa dini inayoendelea kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam ambayo imeandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). 

Aliongeza kuwa viongozi wa dini si wanaharakati bali ni watu wanaotoa uamuzi wao kwa hekima huku wakiaminiwa na wafuasi wao wakiwemo viongozi wa serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga amesema wameandaa semina hiyo kwa ajili ya viongozi wa dini kwa kuwa ni watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii ili kusukuma mchakato wa katiba mpya.

"Semina hii kwa viongozi hawa wa dini ni maazimio yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa dini katika mkutano wa kwanza tulioufanya ambapo walitushauri tuendeshe semina kama hii kwa viongozi wa dini kutoka sehemu mbalimbali nchini ili kuwajengea uelewa mpana wa kujua masuala ya Katiba," alisema Henga.

Mtoa mada katika Semina hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk.James Jese alisema kuna umuhimu wa sheria iliyopitishwa kuelekea upigaji wa kura ya maoni ya katiba mpya ifanyiwe marekebisho kwa kuwa imepitwa na wakati.

Mwenyekiti wa Taifa wa Wanawake wa Baraza la Kiislam Tanzania (Bakwata), Shamim Khan, amesema Rais John Magufuli ameanza kuliongoza taifa kwa  weledi mkubwa hivyo ni vema amalize pia mchakato wa kupata Katiba Mpya. 



No comments: