ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 25, 2017

MKWASA WA YOUNG AFRICANS AVAA RASMI VIATU VYA DR. JONAS TIBOROHA


Hali ya uchumi imebedilika sana, sio kwa Yanga pekee! Kwani hata kwa watani zao ambao ndio sisi sasa teh teh teh hali ni tete kusema kweli, hili la Simba tutalizungumza wakati mwingine tukipata nafasi inshaallah, leo tuongelee Yanga.

Klabu ya Young Africans “Yanga” imezindua rasmi mpango wa kukuza na kuinua uchumi wa Klabu yao kwa kutoa fursa kubwa na pana kwa washabiki na wanachama kuchangia fedha katika account maalumu zitakazotumika kuendesha timu hiyo.

Mpango huu sio mpya katika Klabu hii, Katibu Mkuu wa zamani wa wanajangwani hao Dr. Jonas Tiboroha aliandika Project proposal na kumkabidhi Mwenyekiti, na Selcom walikuwa tayari wamekubaliana na wazo hili na walimhakikishia Dr. Tiboroha kwamba watafanya kazi pamoja, pia akawa amefanya mazungumzo na makampuni matatu ya simu ili kurahisisha mchakato huu. Kila kitu kilikwama kwa mwenyekiti, hakutaka kabisa kusikia jambo kama hili na lilimkera kuona kwamba Yanga wanakwenda kujitegemea na yeye atakuwa sio wa muhimu tena.

Kama zilivyo timu nyingine, Yanga hapo awali ilikuwa ikichangiwa na wanachama tu katika mfumo wa kadi, na kwa kiwango chenye ukomo. Ukitazama idadi ya wanachama sio kubwa sana na hivyo kiasi cha fedha kilichokuwa kikikusanywa hakikukidhi mahitaji na pengine haikuwa fedha inayoweza kufanya jambo lolote.

Tunaweza tukawabeza Yanga na kuwaita kila aina ya majina, lakini kama kuna kitu timu za Tanzania zilitakiwa kufanya miaka mingi iliyopita basi kilikuwa ni hiki. Yanga wamechelewa sana kuingia katika huu uataratibu, na nina hakika wengine watafuata.

Tunaposema Klabu ni kubwa na inaweza ikafanyiwa uwekezaji wa mabilioni ya pesa, kwanza huwa tunatazama rasilimali zake zote, kwa maana ya jina (brand),mali na watu. Sasa ili kuwa na thamani kubwa kiasi hata cha kupandisha bei ya uwekezaji, lazima ujioneshe kama unaweza kuishi bila msaada.

Klabu hii imekuwa ikinyanyasika sana wakati Mwenyekiti wao alipokuwa akijitishia kujitoa, na hakika amewanyanyasa sana! Walipiga mpaka magoti kumlilia asiondoke, waliandamana kuhakikisha anabaki, sio kwamba walikuwa wanampenda sana, thubutuuuu!! Walichokuwa wanakiona ni msaada wake kwa timu. Jambo hili liliwaumiza watu wengi wenye mapenzi na Yanga akiwamo Dr. Tiboroha

Yanga walitengenezewa mfumo tegemezi na wakaukumbatia, waliamini peke yao hawataweza, waliamini bila mwenyekiti basi itashindikana, lakini sio kweli! Ni watu wachache walilazimishwa kufikiria hivyo na kuambukiza wengine, nao wakawaambukiza wenzao, hata wale walioamini wanaweza bila mwenyekiti wakadhani pengine hawa wengi wapo sahihi, na waliwafuata.

Baada kuonekana “anajifanya mjuaji sana”, Dr. Jonas Tiboroha (Mimi peke yangu nchi hii nimeruhusiwa kumuita - Sir. Nkurumbi) alisusiwa timu hii kwa miezi mitatu bila kupewa fedha kutoka sehemu yeyote, hakuna Mwanayanga anajua hii kitu na kama wapo basi ni wachache sana.

Yule bwana alimsusia Tiboroha timu ili ashindwe kuiendesha, na kumuonesha kwamba kafeli lakini haikuwa hivyo! Badala yake utitiri wa makampuni ukaanza kutitirika Jangwani wakitaka kuwekeza, kitu ambacho “bosi kubwa” na watu wake walikiona kama kiyama, kilichotokea baadae kwa Dr. Tiboroha tunakikumbuka vizuri. Kosa lake lilikuwa ni kuhakikisha Yanga inajitegemea na inajiendesha yenyewe kwa fedha zake!!

Charles Boniface Mkwasa “Master” hakika hatosahaulika kwa kuweka mpango huu hadharani, Tiboroha atakumbukwa kwa kuweka mpango huu mezani, ilitakiwa Yanga wapate katibu mkuu mwenye uthubutu atakeyeamini katika uchumi wa kujitegemea, haitajalisha itakuwa ni ngumu kiasi gani lakini angalau wapate fedha zao na waache kunyanyasika.. hongereni sana.

Shaka moja tu ni kwamba, Mkwasa amekuta mpango huu mezani ambao ulikataliwa na kupingwa vikali na mwenyekiti, sasa unatekelezwa chini ya mwenyekiti aliyeukataa. Labda pengine tuseme Mwenyekiti sasa yupo radhi kuona Yanga inajiendesha, na sitaki kabisa kuamini hata kwa sekunde moja kwamba anataka kujilipa madeni yake yote anayoidai Yanga ambayo aliyaainisha wakati wa mapendekezo ya kuikodisha timu, ambao uligonga mwamba.

Naunga mkono juhudi hizi za Yanga, ni vema kujaribu ili muone mtakwama wapi na nina amini watakuja watu kusaidia na mtasimama imara mkiwa Klabu tajiri kabisa Afrika Mashariki.

TUFANYE MAGAZIJUTO KIDOGO (wenye allergy na hesabu mtusamehe)

Yanga inakadiriwa kuwa na wafuasi (wanachama na washabiki) karibu Milioni 8 nchi nzima. Sasa hebu tuachane na takwimu hizi ambazo zitatuchelewesha sana, tuchukue uhalisia wa wanachama na washabiki wanaoweza kuchangia timu yao. Uhalisia huu tunaupata kwenye mashindano ya “Mtani Jembe” ambapo washabiki walipiga kura kwa ajili ya timu zao (at least wenye access na simu za mkononi na ujuzi wa kutumia katika malipo)

Katika Mtani Jembe, Yanga ilipigiwa kura zaidi ya milioni 14, ikiwa na maana kwamba shabiki mmoja aliweza kupiga kura zaidi ya moja, ambayo ni sawa kabisa na mfumo huu wa uchangiaji ambapo shabiki mmoja anaweza kuchangia zaidi ya mara moja na kiwango chochote apendacho kisichopungua Shilingi 1000.

Sasa hebu tufanye Tanzania nzima wapatikane washabiki milioni moja tu kila mwezi, na wachangie shilingi elfu moja tu kila mmoja. Hii itakuwa..

1,000,000 x 1,000 = 1,000,000,000
Hii ni shilingi bilioni moja ya Tanzania kwa mwezi mmoja.
Mwaka mmoja una jumla ya miezi 12, hivyo basi chukua..
1,000,000,000 x 12 = 12,000,000,000
Hii ni shilingi bilioni 12 kwa mwaka mmoja tu.

Na hapo ikumbukwe shabiki mmoja anaweza kuchangia zaidi ya mara moja, na anaweza kuchangia zaidi ya shilingi elfu 1000.

Yanga peke yake kwa mwaka makadirio ya chini kabisa yaani wamekosa saaana wanaweza kukusanya zaidi ya bilioni 15.

Hivi tunashindwa wapi??? Ya nini kujidhalilisha na vipesa vya wadhamini mbuzi eti milioni 500 huku wanakuja na masharti kibao kama waganga wa kienyeji? Yanga mkithubutu wallahy mnatusua maanina zenu.

Ifike wakati sasa kila mwenye mapenzi na timu yake achangie, mlikuwa mnaumia mkisikia mishahara haijalipwa au timu imeshindwa kusafiri, sasa jukumu lipo mikononi mwenu. Na kwa kufanya hivi, hata mkipata mdhamini kwakweli itabidi ajipange sana maana thamani ya Yanga itakuwa sana kuliko kawaida, na huu ni mwanzo tu wa hesabu za wanachama, bado hujaweka fedha zingine kutoka maeneo mbalimbali kama haki za matangazo, udhamini wa ligi, mapato ya getini na kadhalika.

Itakuwa ni fahari kwa kampuni kumdhamini mchezaji wa Yanga kwa pesa nyingi kwasababu Klabu yake itakuwa imemheshimisha, hapo sasa mnaweza kuongea na Nike, Puma, Addidas nk katika mikataba ya kutengeneza jezi ambazo pia mtaziuza kwa wanachama wenu kupitia matawi yenu, hivi Yanga ikifanya hii ndoto kuwa kweli, kuna timu hapa Afrika inayojitegemea ikawa Tajiri namna hii?? Timu nyingi tajiri Africa sio za wanachama, unakuta ni za taasisi au watu binafsi, Yanga inaweza kuwa ya kwanza… tatizo sasa kwenye pesa sisi ndugu watanzania tunajijua wenyewe.

ANGALIZO KWENU YOUNG AFRICANS

Changamoto za kujitegemea ni kubwa sana, hasa ukiweza kufuta utegemezi kwa kujikwamua mwenyewe. Wapo watu hawatafurahiswa na hili kwa sababu zao binafsi, watafanya kila juhudi kuhakikisha mpango huu haufanikiwi kwa asilimia mia moja. Wapo kutoka ndani ya Klabu na wengine nje ya Klabu, hawatapenda Yanga iwe kama mnavyotamani iwe.

Rai yangu kwenu, hakikisheni ipo nia safi juu ya mchakato huu, na unasimamiwa na watu safi wenye mapenzi mema na Klabu yenu. Kwa umoja wenu mnaweza kuandika historia itakayodumu vizazi na vizazi, mtakuwa mfano wa kuigwa na mtasaidia sana kubadilisha soka la nchi yetu.

Mpira ni biashara, kuna faida na hasara, kutoa sadaka na kafara, amueni kusuka au kipara!

Kila la kheri watani zangu wa jadi, Dar es Salaam Young Africans!!

Jeff Gemo Mnyama Machine
The One Man Army
Affirmative Gemo The Great!


1 comment:

Gr said...

Naombeni namba ya Bonifas Mkwasa. Nataka niongee nae private. Unaweza kumpa number yangu +18707538634.