Advertisements

Wednesday, April 26, 2017

Mlimbwende wa bongo azua tafrani bungeni

Mlimbwende wa Tanzania ‘Super Model’, Asha Mabula

By Reginald Miruko, Mwananchi rmiruko@mwananchi.co.tz

Dodoma. Mlimbwende wa Tanzania ‘Super Model’, Asha Mabula anayekwenda kuiwakilisha Tanzania katika shindano la dunia la urembo jijini Macau, China jana alitambulishwa bungeni na kuzua mjadala mzito kuhusu kuchangiwa fedha kwenda katika mashindano hayo.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, jana asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alimtambulisha mrembo huyo miongoni mwa wageni waliokuwa bungeni jana.

Baadaye, Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta alisimama kuomba muongozi wa spika, kuhusu haja ya wabunge kumchangia fedha, walau Sh30,000 kutoka kwa kila mmoja ili mrembo huyo aweze kusafiri kwenda China kuwakilisha taifa.

Alisema hilo ni tukio kubwa hata timu ya taifa ilipokwenda Bungeni ilichangiwa na hivyo akatoa hoja kuomba wabunge wamchangie.

Kutokana na hoja hiyo, Mwenyekiti Chenge alitoa fursa kwa wabunge kujadili suala hilo kwa ufupi na wakatikea baadhi ya wabunge wakipinga huku wengine wakiunga mkono.

Akichangia hoja hiyo, Cosato Chumi wa Mufindi Mjini, alisema hoja ya Sitta ilikuwa ya msingi na kuwa umekuwa utamaduni wa kawaida kwa wabunge kuwachangi wanamichezo wanaofanya vizuri na kutembelea bunge.

Alisema hata timu ya taifa ya vijana ilipotembelea Bunge na mwanariadha Felix Simbu walichangiwa, hivyo Mama Sitta aungwe mkono na kumchangia mlimbwende huyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata alisema wabunge wanapata kadi nyingi za kuchangia mambo mbalimbali zikiwamo harusi na wanachanga na hivyo hawakuwa na sababu ya kukataa kumchangia mrembo huyo.

Alisema anajisikia vibaya kuona wabunge wanawake ndiyo wanaoongoza katika wanopinga kumchangia mwanamke mwenzao, alipendekeza anayetaka kuchanga achange na asiyateka aache.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy aliungana na Mlata akusema kuwa anayetaka kuchanga afanye hivyo asiyetaka aache na kuwa yeye ni mmoja ambaye hatachanga.

Mbunge wa singida mashariki, Tundu Lissu alisema ni jambo jema sana kumchangia Mrembo, lakini wananchi wa jimbo lake wana njaa na Rais John Magufuli amekataa katakata kutoa chakula cha msaada, hivyo ni bora kuwachangia wenye njaa na huyo mlimbwende asubiri.

Ally Salehe, mbunge wa Malindi alieleza kumshangaa mbunge aliyesema wanawake wawe na huruma, huku akihojia mbona hawakuwa na huruma na kupotea kwa Ben Sanane, jambo ambalo Mwenyekiti Chenge alimkataza akitaka ajielekeze kwenye hoja iliyoko mezani.

Baada ya mjadala huo, Chenge aliamua kuwahoji wabunge huku zikisikika sauti mbalimbali na kushindania suala hilo, lakini alipowahoji alisema anaamini walioafiki kumchangia mlimbwenda huyo wameshinda.

No comments: