ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 23, 2017

MSANII WA BONGO FLEVA 'NILLAN' AMPONDA SHILOLE KWA KUHARIBU SHOW SIKUKUU YA PASAKA

Na Mwandishi Wetu

MSANII wa Bongofleva anayetamba na kibao cha ‘Njenje’ Gilbert Paul maarufu kama ‘NILLAN’ (pichani kulia) ameponda kitendo kilichofanywa na msanii  mkubwa katika  tasnia hiyo Zuwena Yusufu ‘Shilole’ cha  kuharibu Show iliyotarajiwa kufanyika mkesha wa siku ya mkesha wa Pasaka na hivyo kusababisha hasara kwa promota.

Nillan aliyetarajiwa kufanya show siku pamoja na msanii mwingine Nuhu Mziwanda alisema kitendo kilichofanywa na Shilole siyo cha kiungwana kutokana na heshima kubwa aliyonayo msanii huyo kwa Taifa hili.

“Ukweli kitendo hicho mimi kama msanii chipukizi kimeniumiza sana, sikutaraji kingeweza kufanywa na msanii mkubwa na maarufu kama Shishi, namuheshimu kama dada yangu lakini kwa hili amejishushia heshima” alisema Nillan.

Show hiyo iliyokuwa imeandaliwa na Kampuni ya  Merry Merry Entertainment, ilishindwa kufanyika baada ya Shilole kuchelewa kufika ukumbini hali iliyosababaisha mashabiki waliofika mahali hapo kulalamika warudishiwe fedha zao na baadae kuondoka.

Akizungumzia baada ya tukio hilo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Merry Mussa mbali na kulaani kitendo hicho cha Shilole alisema  ni lazima sharia itafuata mkondo wake kwa msanii huyo kulipa hasara yote iliyotokana na kitendo alichokifanya.


“Haiwezekani mtu tukubaliane afike  ukumbini saa  2 usiku, yeye anakuja  muda anaotaka, na hapo hapo hata kushuka kwenye gari hakushuka, hiyo ni dharau na kamwe sikubaliani na kitendo hicho hata kidogo” alisema Merry.

Shilole aliyetarajiwa kutoa burudani  siku hiyo ya mkesha wa Pasaka katika ukumbi wa Heinken uliopo Kijichi, aliwasili ukumbini hapo saa 7 za usiku tofauti na makubaliano na Promota aliyeandaa show hiyo.

Hata hivyo alipotafutwa Shilole kuzungumzia suala hilo alidai kufika ukumbini hapo kama taratibu zilivyo za wasanii kufika kwenye show mbalimbali hivyo haoni kama kuna kosa lolote alilifanya kuhusiana na show hiyo.
Kwa upande wake Nuhu Mziwanda aliyewah kuwa mahusiano na msanii huyo alikwenda mbali na kusema kitendo kilichofanywa na mpenzi wake huyo wa zamani ni ushamba na kumtaka kurudisha fedha alizochukua kutoka kwa promota.
Alisema anashangazwa kwanini Shilole alikubali kupokea fedha hizo na kuahidi kufanya show lakini badala yake akaingia mitini na kuibukia ukumbini muda ambayo show ilipaswa iwe mwishoni.


Akizungumzia suala hilo Meneja wa kampuni ya Ochu Entertainment  inayomsimamia msanii Nillan, Felix Mkuya alisema kitendo kilichofanywa na Shilole ni cha kushangaza na hakipaswi kufanywa na  wasanii wa hapa nchini.

“Imagine watu wametumia gharama kubwa kuandaa ile Show, kila msanii alishapewa hela yake mkononi, sasa kwanini yeye afanye vile, Nuhu Mziwanda alifika ukumbini mapema saa 12 jioni, alikadhalika kwa Nillan…sasa vipi Shilole afanye vile” alihoji Mkuya.

No comments: