Mgombea wa nafasi ya uongozi kwenye Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ngazi ya tawi, Halima Saidi Haji.
Stori: Boniphace Ngumije na Mayasa Mariwata |Risasi Jumamosi| Habari
DAR ES SALAAM: Binadamu akipanga yake na Mungu anapanga yake! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia tukio la mgombea wa nafasi ya uongozi kwenye Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ngazi ya tawi, Halima Saidi Haji, mkazi wa Magomeni Kagera kufariki dunia akiwa katika nyumba ya kulala wageni ‘gesti’ iliyopo mtaani kwake, hivyo kifo chake kufuta kila kitu.
Akizungumza na Risasi Jumamosi kwa simanzi kubwa, mtoto mkubwa wa marehemu, Rehema alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa, kwa mara ya mwisho alionana na mama yake Jumapili ya Pasaka, majira ya saa 10 jioni.
SIKIA USHUHUDA
“Siku hiyo, mama aliniambia kuwa atatoka jioni hiyo kwenda kwenye matembezi yake, lakini baada ya kutoka mpaka muda ya saa 6 usiku hakuwa amerejea nyumbani. Mimi nilishikwa na wasiwasi maana haikuwa kawaida yake mpaka kufika muda huo hajatoa taarifa alipo.
“Ilipofika saa 7 za usiku huohuo, nikaamua kumpigia simu, alipokea na ilionekana alikuwa kwenye eneo lenye kelele kwa hiyo hatukusikilizana vizuri, ila kwa kuwa ilikuwa ni sikukuu na nilimsikia sauti yake akiwa salama sikujali, nilijua yupo kwenye mambo yake na angerudi nyumbani,” alisema Rehema.
TAARIFA ZA KIFO
Rehema aliongeza kuwa, aliamua kulala, na kulipopambazuka alimpigia simu mama yake bila kumpata hewani ambapo katika hali asiyoitegemea, majira ya jioni alipata taarifa kwamba, mama yake alikutwa amekufa kwenye gesti hiyo.
BABA WA MAREHEMU HUYU HAPA
Kwa upande wa baba mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Juma Kaniki alisema taarifa juu ya kutokea kwa kifo hicho alizipata kutoka kwa jamaa zake wa karibu majira ya jioni, Jumatatu iliyopita (Jumatatu ya Pasaka) akiwa kwenye mishemishe zake.
“Kiukweli sikuweza kuziamini moja kwa moja, nikaamua kukimbia mpaka Hospitali ya Taifa Muhimbili na baada ya kujieleza niliruhusiwa kwenda mochwari kuutambua mwili wa mwanangu. Baada ya kufika na kuutazama nilikuta ndiye mwenyewe.
“Nilisikitika sana, ikabidi kurudi nyumbani na kuungana na ndugu wengine kwenye msiba. Hata hivyo, baada ya kufika niliamua kwenda kwenye hiyo gesti kuhoji nini kilitokea mpaka umauti ukamkuta mwanangu,” alisimulia Kaniki.
Akaendelea: “Nilipohoji, mhudumu aliyekuwa zamu aliniambia kuwa alimpokea marehemu amiwa ameongozana na mwanaume usiku wa majira ya kama saa nane hivi.”
MTUHUHUMIWA WA KUUA ALIOMBA CHAJA!
“Baada ya kufika, walilipia chumba na kuingia ndani, lakini muda kidogo yule mwanaume alirudi mapokezi na kuomba chaja. Yule mhudumu alimwambia taratibu zao za gesti hawaruhusu mtu kuomba chaja na kwenda kuchajia simu chumbani, wakamtaka aache simu mapokezi hapo aweze kuchajiwa.
MTUHUMIWA WA KUUA ALIPIA SIKU YA PILI
“Lakini yule jamaa alikataa na kurudi chumbani na hakuna aliyejua kilichoendelea mpaka kulipopambazuka. Yule mhudumu aliendelea kunieleza kuwa, asubuhi hiyo, yule mwanaume alifika mapokezi na kusema mpenzi wake alikuwa amepumzika na asingependa asumbuliwe, akalipia gharama ya chumba kwa siku hiyo (Jumatatu) na kuwataka wamuache akiamka atatoka mwenyewe.”
MWILI WAGUNDULIWA, UMEFUNIKWA SHUKA
Mzee Kaniki aliendelea kusema kuwa, saa zilizidi kukatika bila mwanamke huyo kutoka chuumbani wala kuomba maji jambo lililowapa maswali wahudumu hao hivyo, ilipofika mchana kama saa nane, mhudumu mmoja akaamua kwenda kugonga mlango na baada ya kutojibiwa, aliufungua kwa nguvu na kuingia ndani ambapo alimkuta Halima amelala sakafuni huku amefunikwa shuka na kitandani pakionekana hapakulaliwa kabisa.
“Baada ya mhudumu huyo kuona hali hiyo alimuita meneja wake ambaye alitoa taarifa polisi na baada ya polisi kufika waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Muhimbili kwa ajili ya taratibu zingine za kipolisi,” alimaliza mzee Kaniki.
MASWALI KIBAO
Baadhi ya waombolezaji walishangaa kusikia mwili wa marehemu ulikutwa sakafuni ukiwa hauna majeraha wala kiashiria chochote kwamba, aliuawa hivyo wangi kuuliza nani alimuua? Au alikufa mwenyewe?
Baadhi ya waombolezaji walisikika wakiseka kuwa, mwanaume aliyedaiwa kuwa na marehemu alikuwa akionekana kubadili nguo kila mara lakini watu wa mtaani walisema hawajawahi kumwona eneo hilo.
Wengi walisema kuwa, mwanaume huyo huenda alikusudia kufanya unyama huo na kukimbia kwani hata funguo za mlango wa gesti hiyo zilikutwa kwa juu huku mlango ukiwa haujafungwa na funguo hali iliyoacha wasiwasi kwamba huenda kulikuwa na kisasi.
MWENYEKITI WA MTAA AMLILIA
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Jangilaga alisema amesikitishwa mno na kifo cha Halima kwa sababu alikuwa ni mmoja wa wajumbe muhimu kwenye kamati ya serikali ya mtaa lakini pia alikuwa akigombea uongozi wa U.W.T katika ngazi ya tawi (Risasi Jumamosi lina nakala ya fomu ya kugombea).
“Kiukweli mama Rehema alikuwa ni mtu muhimu mno kwenye kamati ya serikali ya mtaa. Kifo chake kimeniuma sana, huwezi amini Jumatano tu (Aprili 12) tumetoka kumuhoji juu ya kugombea kwake U.W.T na Jumamosi hii, (Aprili 22) alitakiwa kuhojiwa tena lakini ndiyo hivyo tena kaondoka,” alisema Jangilaga.
SIFA YAKE KUU
Kwa mujibu wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho, U.W.T ni jumuiya yake, marehemu alikuwa tegemeo kubwa wakati wa chaguzi mbalimbali za chama hicho mwaka 2012 na alitegemea kuwa hivyo, mwaka huu ambapo chama hicho kitakuwa na chaguzi kuanzia ngazi ya taifa.
Walisema kuwa, marehemu alimudu vyema kupiga debe wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kiasi kwamba, wanaamini ushindi wa kura za urais na ubunge wa eneo hilo, marehemu alikuwa na mchango mkubwa.
WATU WAFURIKA KUUAGA MWILI
Baada ya taratibu za awali za kipolisi kukamilika, Jumatano iliyopita mamia ya wakazi wa Mtaa Magomeni Kagera na sehemu mbalimbali za jiji walifurika nyumbani kwa marehemu kuuaga mwili wake ambao ulisafirishwa Muheza mkoani Tanga kwa mazishi, juzi Alhamisi.
MENEJA WA GESTI NA RISASI JUMAMOSI
Juzi, Risasi Jumamosi lilimpigia simu meneja wa gesti hiyo baada ya kumkosa kazini kwake ambapo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Ila siko sehemu nzuri kwa sasa, hivyo siwezi kusema sana.”
Mbali na kaucha simanzi kwenye jamii yake, marehemu Halima ameacha watoto watano huku mumewe akiwa alishafariki dunia miaka kadhaa iliyopita.
GPL
No comments:
Post a Comment