ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 28, 2017

WAKAZI WA OLASITI JIJINI ARUSHA WASUSIA MAJI WASEMA HAYANA LADHA ,HAYAFAI KWA MATUMIZI YEYOTE

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Olasiti kama wanavyoonekana  pichani.Picha na Vero Ignatus blog.

Na .Vero Ignatus,Arusha.
WAKAZI wa Olasiti jijini Arusha wamesusia maji yanayotolewa na Idara ya maji na kudai kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya aina yoyote.

Wakizungumza  katika mkutano wa hadhara uliofanywa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo wananchi hao walisema maji yaliyosambazwa na Idara ya maji yana  chumvi kiasi cha kuharibu  hata mimea wanapojaribu kumwagilia.

Mmoja wa wakazi hao Meck  Mollel alisema wanahofia baada ya miaka ijayo kutokuwa na nguvu za kiume kutokana na kuendelea kutumia maji hayo ambayo yanaladha ya magadi.

"Kweli haya maji yanatupa hofu baadaye tutajikuta wanawake wote kwa mpango huu hatuyahitaji haya maji tuleteeni maji yaliyorafiki kwa binadamu" alisema Mollel.


Naye mkazi  mwingine alisema maji hayo akiwapa vifaranga wanapata matege kutokana na hali ya chunvi iliyozidi ambapo pia alisema akimwagilia mimea inakuwa ya njano.

Hata hivyo mkuu wa mkoa aliwataka wananchi hao kufahamu kuwa serikali haiwezi  kuruhusu maji yasiyo faa kwa matumizi ya binadamu  hivyo maji hayo yalipimwa na kuonekana yanafaa ndio maana yakaruhusiwa.

"Serikali  yoyote duniani haiwezi  kuruhusu kitu chenye madhara kwa wananchi wake hivyo  tutaleta tena wataalamu  kuyapima  tena na majibu yatakayopatikana  tutajua cha kufanya" alisema Gambo.

Naye Mkurugenzi wa maji jiji la  Arusha Ruth Koya alisema  kiwango cha maji salama hakipimwi kwa macho  bali  kinapimwa maabara  hivyo wataalam wamepima na wakaona yanafaa kwa matumizi.

Koya alisema maji wanayolilia wananchi hao yanafloride lakini hayo yaliyopo pamoja na kuwa na chumvi hayana madhara kwa matumizi Kama wanavyolalamika wao..

No comments: