ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 23, 2017

DC UBUNGO MHE KISARE MAKORI AAGIZA KUJENGWA DARAJA LA MBEZI MSUMI

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori akisikiliza malalamiko ya wananchi wa Mtaa wa Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam wakielezea adha wanayokumbana nayo kutokana na uharibifu wa Daraja
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori  sambamba na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg Ally Ally wakikagua daraja lililovunjika eneo la Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam.

Muonekano wa Daraja la Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam likiwa limeharibika
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam
 
Na Nasri Bakari, Dar es salaam

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori Leo Jumamosi, Mei 20, 2017 ameagiza kujengwa kwa daraja  jipya kutokana na kuharibika kwa daraja la awali katika eneo la Msumi Kata ya Mbezi Jijini Dar es salaam.

Agizo hilo amelitoa mapema hii leo wakati akizungumza Na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa Hadhara uliowajumuisha pia Mtendaji wa Kata,  wajumbe wa mitaa na wataalamu mbalimbali kutoka Manispaa ya Ubungo.

Mhe Makori amesema kuwa amejionea adha  iliyopo katika daraja hilo ambapo sio ubovu wa miundombinu pekee bali pia ni swala la usalama hasa kwa watoto wanaopita katika daraja hilo waendapo shuleni na sehemu mbalimbali.

"Mimi kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika Wilaya hii sitojisikia vizuri kuona tunahatarisha maisha ya binadamu kwa namna yoyote ile, lazima nihakikishe mnakuwa salama wakati wote" 

"Hivyo nakuagiza Mkurugenzi kuanza haraka ujenzi wa daraja hili ambalo kwa kiasi kikubwa litasaidi wananchi Wetu hawa  kupita kwa usalama zaidi" Alisema Mhe Makori.

Aidha amesisitiza kuwa kodi zinazokusanywa na serikali  ni kwa ajili ya kugharamia na kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kama vile kuboresha Sekta ya Elimu, Afya na huduma nyingine za kijamii, hivyo ni lazima  serikali ishughulikie na kusimamia mahitaji ya Msingi kwa wananchi wake.

Sambamba na hayo pia Mhe Makori amewaomba wananchi kufika kwa viongozi wao pindi wanapopata kadhia mbalimbali zinazowasumbua katika jamii inayowazunguka kwani wameajiriwa kwa ajili yao na serikali ya awamu ya tano inajali wananchi wote hususani wanyonge.

Kwa upande wake Injinia wa Ujenzi Manispaa ya Ubungo Ndg Goodluck Mbanga amesema kuwa daraja lililokuwa limejengwa awali lilikuwa Dogo ukilinganisha Na wingi wa Maji Jambo lililopelekea kuharibika haraka.

Mbanga Alisema utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya nitaanza haraka iwezekanavyo ili kufikia mwanzoni mwa mwaka 2018 lianze kutumiwa Na wananchi hao ambao wamepata adha kubwa kwa muda mrefu.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Msumi Ndg Hemed Abdallah Gulamu amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kwa Kazi kubwa anayoifanya tangu alipoteuliwa kuongoza Wilaya hiyo.
Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa ufanisi katika utendaji Na kusema kuwa uongozi wake utaacha alama kubwa na kukumbukwa na watanzania wote.

MWISHO

No comments: