Advertisements

Saturday, May 13, 2017

DIMBWI LA MAHABA: Dalili za kumjua mwanamume wa maisha yako

NI vyema sasa wanawake wakajifunza kuacha kabisa, kuwaulizauliza wenza wao juu ya suala la ndoa, kwani mara nyingi hali hiyo huwatisha wanaume na hawaipendi kabisa. Si ajabu kumsikia mwanamume anabainisha wazi kuwa hataki mwanamke anayemsumbuasumbua kuhusu suala la ndoa, na kwamba kama yuko tayari kumuoa atamuambia.

Sasa ili wanawake waepuke kero hii ambayo mara nyingi huwakimbiza wanaume au kuufanya uhusiano kuwa mchungu, ni vyema wakajifunza kuzisoma dalili za mwanamume mwenye nia ya kweli ya ndoa na si wa kupita tu.

Dalili hizo mara nyingi ni chache na huenda mwanamume akakuonesha dalili moja kati ya hizo na hiyo haimaanishi kuwa tayari amekuchagua kuwa mwenza wake wa maisha. Moja ya dalili ambayo huenda mwanamume ana nia ya dhati ya kuwa na maisha ya ndoa na mwenza aliyenaye ni pamoja anapotumia vipindi vyake vya likizo na mwenza wake huyo.

Ukiona mwanamume wako anajitolea kutumia muda wake wa mapumziko au muda ambao angeutumia na familia yake na kusafiri au kukufuata uliko hata kama ni mbali, ujue kuwa mwanamume huyo anafikiria kujenga maisha ya baadaye na wewe.

Lakini endapo mwenza wako akianza tabia ya kutengeneza stori kila pale anapopata mapumziko na kutumia muda mwingi wa likizo yake na marafiki zake hadi pale utakapomfuata wewe, jiulize mara mbili kuhusu uhusiano huo.

Dalili nyingine ni pale mwenza wako huyo wa kiume anapoongozana na wewe kwenye sherehe za familia yake au marafiki zake. Ni mara chache sana mwanamume kwenda na mwanamke ambaye hana nia naye ya maisha ya baadaye na kumuon esha mbele ya familia yake, anapochukua hatua ya kuongozana naye ujue tayari anafikiria suala la ndoa.

Pamoja na hayo, mara nyingi mwanamume aliyeanza kufikiria kuanzisha familia na mwenza wake, katika mazungumzo yake yanayohusu maisha kama vile watoto, nyumba au masuala ya maendeleo, lazima amshirikishe au kumuingiza mwenza aliyenaye.

Epuka sana na kuwa makini unapokuwa kwenye uhusiano na mwanamume, asiyezungumzia jambo lolote la maendeleo au maisha yake ya baadaye halafu baadaye unashtukia tu amenunua kiwanja, anajenga au amenunua gari.

Pia dalili nyingine za mwenza wa kiume anayefikiria kujenga maisha ya baadaye na mwenza wake ni kumshirikisha na kumuomba ushauri katika masuala yake binafsi asioweza kumwambia hata rafiki yake, kama vile migogoro ya kikazi au kifamilia.

Mara nyingi mwanamume wa hivi huweza hata kuonyesha hisia zake pale anaposikia huzuni au hasira ikiwemo hata kulia mbele ya mwenza wake huyo kwa kuwa tayari ameshajenga katika fikra zake kuwa huyo ndio mwenza wa maisha yake, atakayeishi naye kwa shida na raha

HABARI LEO

No comments: