Advertisements

Saturday, May 13, 2017

MKUU WA MKOA AAGIZA POLISI KUKAGUA MABASI YA WANAFUNZI

Serikali  mkoani Kilimanjaro imeagiza jeshi la polisi mkoani hapa, kufanya ukaguzi maalumu wa magari yanayobeba wanafunzi hususani shule binafsi ili kujiridhisha kama yana sifa ya kufanya kazi hiyo.

Mkuu wa mkoa huo, Saidi Mecki Sadiki alisema hayo wakati wa Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) ambacho kilikuwa maalumu kwa suala la hifadhi ya mazingira. 

“Kikosi cha usalama barabarani kiandae mpango wa ukaguzi wa magari ya wanafunzi kila Jumamosi na yale yasiyo na sifa yaondolewe barabarani....hatuwezi kukaa kimya huku tunaendelea kupoteza maisha ya watoto wetu kama ilivyotokea mkoani Arusha” alisema.
Sadiki alisema Serikali ilisikitishwa na vifo vya watu wasio na hatia kwani pia katika ajali hiyo mkoa wake uliguswa kwa kupoteza watoto 14. Alimtaka Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issa kusimamia kikamilifu ukaguzi huo ili kuepuka udanganyifu.

Ajali ya basi la shule Lucky Vicent ilitokea Mei 6, 2017 katika eneo la Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha na kusababisha vifo vya wanafunzi 32 pamoja na walimu wawili na dereva wa basi hilo.

Jeshi la polisi mkoani Arusha tayari limeeleza chanzo cha ajali kuwa pamoja na mwendo kasi, lakini pia wanafunzi na walimu hawakuwa wamefunga mikanda jambo ambalo lingepunguza athari za ajali. 

Aidha, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema pia gari hilo lililokuwa na uwezo wa kubeba watu 30, lilibeba 38 kinyume na uwezo wake

No comments: