Advertisements

Monday, May 22, 2017

Rais wa TFF atoa pongezi kwa Mh. Sima

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ametuma salamu za pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida ulioingia madaraka jana Mei 20, 2017.
Mbunge wa Singida Mjini, Mheshimiwa Mussa Sima amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa SIREFA baada ya kuwashinda wenzake Erasto Sima, Hussein Mwamba, Said Mnyampanda na Samwel Nakei.

Katika salamu zake kwa SIREFA, Rais Malinzi amesema anashukuru kwa uamuzi wa kidemokrasia uliofanywa na wajumbe wa mkoa huo na kwamba ana imani na uongozi ulioingia madarakani.
“Kwa namna ya wanafamilia wa mpira wa miguu wa Mkoa wa Singida walivyodhamiria kutaka kuleta maendeleo ya mpira wa miguu, nina imani na uongozi wa Mheshimiwa Sima katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya soka mkoani huo,” amesema Malinzi.

Katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) mjini Singida na kusimamiwa na Mwenyekiti Stella Maila, pia ulimchagua Katibu Mkuu Rashid Koba wakati Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF ni Nurfus Ndee huku Hamza Ntoga akichaguliwa kuwa Mweka Hazina Msaidizi.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilikwenda kwa Ally Ramadhani Nkhangaa aliyekuwa mgombea pekee wakati Koba alimshinda Edward Ihonde na Ndee alimshinda Manase Abel.
Uchaguzi wa SIREFA ulifanyika baada ya viongozi wengine walioingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, kujiuzulu kutokana na kubanwa na majukumu mbalimbali.

No comments: