Advertisements

Wednesday, June 21, 2017

Rais Magufuli atuma rambirambi kifo cha Ali Yanga

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametuma rambirambi kwa familia, wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uongozi wa Klabu ya Yanga na wanamichezo wote kwa jumla kutokana na kifo cha shabiki wa Klabu ya Yanga, Ali Mohamed maarufu Ali Yanga.

Ali Yanga amefariki dunia jana (Jumanne), Juni 20 kwa ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Chipogolo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Taarifa iliyotolewa leo (Jumatano) na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imemkariri Rais Magufuli akisema atamkumbuka Ali Yanga kwa uzalendo na mchango wake wa kuhamasisha na kushabikia masuala mbalimbali ya kitaifa na hasa michezo, ikiwamo kuishabikia timu yake ya Yanga, timu ya soka ya Taifa, CCM na shughuli za kiserikali kama vile Mwenge wa Uhuru na ziara za viongozi.

“Nimeguswa sana na kifo cha Ali Yanga, nilikuwa naye wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa wananchi kukipigia kura chama changu cha CCM, pia amekuwa akiongoza mashabiki wenzake kuishabikia timu ya Yanga na timu ya Taifa bila kuchoka. Kwa kweli alikuwa hodari sana katika ushabiki wake,” amesema.

Rais amesema, “Natoa pole nyingi sana kwa familia yake, viongozi wa timu ya Yanga, wanamichezo wote, wana CCM na wote walioguswa na kifo cha Ali Yanga. Namuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi.”

No comments: