ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 29, 2017

RC Mongela -Awapa “Kibano” Wanamichezo

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. John Mongella, akiwa amenyanyua kikombecha Jumla cha UMITASHUMTA juu mara baada yakukabidhiwa.
Picha ya Pamoja baina ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Timu ya UMITASHUMTA ya Mkoa wa Mwanza, walioibuka washindi wa kwanza katika Mashindano hayo.
Binti Chausiku Akimkabidhi Kombe la Jumla Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya wenzanke.
Pichani ni Washindi wa kwanza wa UMITASHUMTA 2017, mkoa wa Mwanza mara baada yakutangazwa na Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako ( Picha zote na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa).

Na. Atley Kuni Mwanza

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, amewataka vijana wanamichezo wa UMITASHUMTA na UMISETA pamoja na walimu wao kujizatiti katika suala zima la taaluma mara baada yakufanya vizuri katika michezo hiyo iliyo malizika mkoani hapa kwa mwaka huu wa 2017 na mkoa huo kuibuka mshinda wa kwanza na wapili.

Mongella ameyasema hayo wakati alipokuwa akiipokea timu ya mkoa wake ya UMITASHUMTA iliyo ibuka mshindi wa jumla mara baada yakumalizika kwa michezo hiyo iliyoshikisha mikoa ishirini na sita (26) ya Tanzania bara.

Ameongeza kuwa, ili Michezo waliyo shinda iwe na maana, hawana budi kujizatiti katika taaluma “Nichukue fursa hii kuwaelekeza kwamba nguvu hii na mshikamano huu ambao tumeuonesha katika michezo uende mbele zaidi, tukajizatiti kwenye masomo, ili tuwe wakwanza katika kila nyanja” alisema Mongella na kuongeza kuwa, yupo tayari kushirikiana nao bega kwa bega katika kuhakikisha mkoa huo unakuwa wa mfano wakuigwa katika sekta zote.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Afisa Elimu wa mkoa huo, Michael Ligola, kumpatia orodha ya wanafunzi wote walishiriki na kutwaa ubingwa huo ili waweze kuingizwa katika mipango ya mkoa.

Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Afisa Elimu wa mkoa wa Mwanza, amesema, kumalizika kwa mashindano hayo ndio mwanzo wa mashindano yajayo sambamba na taaluma. “Mh. Mkuu wa Mkoa, tuliona mara baada yakumalizika kwa mashindano haya sio vizuri waondoke bila kupata maneno ya nasaha kutoka kwako hususan ni katika suala zima la taaluma”

Kwa mujibu wa taarifa ilisomwa mbele ya mkuu wa mkoa na Afisa Elimu Msingi kutoka Wilaya ya Misungwi, Ephrahim Majinge, mkoa wa Mwanza umefanikiwa kuwa mshindi wa jumla kwa upande wa UMITASHUMTA kwa michezo yote, huku ukitwaa vikombe vya Soka wanaume, mshindi wa kwanza, Mpira wa mikono mshindi wa kwanza na Riadha mshindi wa kwanza kitaifa, michezo mingine ni Netball mshindi wa kwanza kitaifa, sambamba na mkoa kushika nafasi ya pili kwa michezo ya Wavu na mpira wa mikono.

Aidha kwa upande wa UMISETA, mkoa wa Mwanza, umeshika nafasi ya pili kitaifa kwa kutwaa vikombe vipatavyo sita kutoka michezo tofauti tofauti, iliyoshikisha timu 28 za mikoa Tanzania bara na Zanzibar.

Mkoa wa mwanza umekuwa mwenyeji wa michezo hiyo kwa mwaka wa 2017, ambapo katika ufunguzi wa michezo hiyo, ulifanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa upande wa UMISETA na kwa upande wa UMITASHUMTA yalifunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene (MB) na kufungwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako.

No comments: