ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 27, 2017

WAISLAMU WATAKIWA KUENDELEZA UCHA MUNGU

Na Swahilivilla Washington Waislamu wametakiwa kuendeleza Ucha Mungu na mema waliyokuwa wakiyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Sheikh Yussuf Mecca, kutoka Columbus, Ohio
Wito huo ulitolewa jana na Sheikh Yussuf Mecca alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za Iddi zilizoandaliwa na Jumuiya ya Waislamu wa Tanzania wa Jiji la Washington na Vitongoji vyake ijulikanayo kwa jina la TAMCO.
"Kwa vile mwezi wa Ramadhani umekwisha isiwe yale yote mazuri tuliyokuwa tunayafanya ikawa ndiyo basi, na tusubiri Ramadhani nyengine" alisema Sheikh Yussuf.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa kujitahidi kumcha Mungu wakati wowote na kujitahidi katika kutenda mambo mema na ibada ili kujiandaa na safari ya Akhera ambayo inanaweza kumfikia mtu wakati wowote.
" Hakuna hata mmoja ambaye anajua ni siku gani atafumba jicho na atakufa", alisisitiza Mgeni huyo rasmi kwenye shere hizo, huku akitilia nguvu hoja yake kwa Aya ya Qur'an isemayo: "كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ" (Kila nafsi itaonja mauti/kifo), akigogoteza kuwa hakuna mtu yoyote anayejua atakufa lini au mahali gani.
Aliongeza kusema kuwa kurejea kwenye maasi baada ya juhudi kubwa za ucha Mungu na ibada katika mwezi wa Ramdhani ni sawa na kuiharibu kazi ya kiufundi liyofumwa kwa juhudi na ustadi mkubwa.
Mwenyekiti wa TAMCO Bwana Ali Muhammed
Sherehe za Iddi za Waislamu wa Tanzania katika Mji huo Mkuu wa Marekani, ni utamaduni ulioanza tangu mwaka 1998, ambapo Waislamu waliona haja ya kuwa na mjumuiko wa pamoja katika Siku Kuu, ikizingitwa kuwa Marekani si nchi ya Kiislamu na kwa hivyo hakuna sherehe rasmi za Iddi, kama alivyoelezea Mwenyekiti wa TAMCO Bwana Ali Muhammed:
"Wazee na vijana waliokuwepo hapa katika miaka hiyo waliona kuna haja ya kuanzisha Umoja ambao utawasaidia katika mambo yao ya Kidini, siyo tu kwenye sherehe za Iddi, bali pia katika maswala mengine ya sherehe na misiba. Na baada ya chombo hicho kuanzishwa ndipo ukaanza utaratibu wa kuandaa sherhe kama hizi za Iddi".
Bwana Ali aliesema kuwa sherehe hizi zinakuja baada ya Mfungo wa Ramadhani ambapo jumuiya yake hukodi ukumbi maalum kwa ajili ya futari ya pamoja kwa wanachama wake na wageni wengine waalikwa kila siku za Jumamosi na Jumapili katika mwezi huo mtukufu.
Aliendelea kusema kuwa sherehe hizi za Iddi hufanyika kwa awamu mbili, asubuhi na jioni: "Mwanzo tulikuwa tunafanya tu sherehe za wakati wa jioni, lakini baadaye tukaona kuna haja ya kukutana pamoja wakati wa asubuhi, kwa vile kuna watu baada ya kutoka Msikitini huwa hawana pa kwenda, kwa hivyo tukaona ni vizuri tuianzie asubuhi ili watu walitoka Msikitini waje hapa wapate chai ya asubuhi na baadaye kurejea tena jioni na kwa hivyo kufanikisha furaha kwa siku nzima ya Iddi"
Akizungumza na Swahilivilla, Mwenyekiti huyo wa TAMCO alidokeza kuwa jumuiya yake imekuwa ikikutana kila baada ya muda fulani ili kupanga mikakati ya kuiendeleza jumuiya hiyo kwa kupitia kamati zake mbali mbali, jambo ambalo limepelekea ufanisi mkubwa na kuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa jumuiya za Watanzia nchini Marekani.
Kama ambavyo penye mafanikio hapakosi changamoto, TAMCO nayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za hapa na pale. Miongini mwao ni uchache wa watu wa kujitolea katika matayarisho ya shughuli za jumuiya na uendeshaji wake kwa ujumla.
Kwa hivyo, kiongozi huyo wa TAMCO amewatolea wito wanajumuiya hiyo kujitokeza kwa wingi katika kujitolea kwenye maandalizi ya shughuli zake na uendeshaji wake kwa ujumla akisema:
"Jumuiya hii ni yetu sote, na tutaiendesha sisi wenyewe, hakuna mtu ambaye atatoka sehemu nyengine kuja kutusaidia kuiendesha, kwa hivyo ni kuweka nia zetu na kuweka umuhimu tukizingatia kuwa chombo hiki ni cha kwetu, basi tufanye jitihada zaidi za kukitunza.
Aidha alikumbusha kuwa TAMCO ni jumuiya inayoendeshwa kutoka na ada na michango ya wanachama wake, na kwamba ni muhimu kwa wanachama kujitahidi katika kutekeza wajibu wao wa kutoa michango yao kwa wakati.
"Inapofika wakati wa kutoa michango tutoe michango, kwani tukifanya hivyo chombo chetu kitakwenda mbali zaidi". Alisistiza Kiranja wa TAMCO, Bwana ali Muhammed.
Sherehe za Iddi za Wasialamu wa Tanzania jijini Washington ni fursa nzuri kwa familia za wanachama wake ambapo hutoa fursa kwa watoto kupata muda na sehemu ya kusherehekea na kujisikia kuwa wako katika Siku Kuu wakiwa Ughaibuni.
Image may contain: 9 people, people smiling, indoor and food
Wa kwanza (kulia) Aziza Mattaka,  Miriam Manu kutoka watatu (kulia) na rafiki zao
Miongoni mwa watoto waliopata nafasi ya kuhudhuria sherehe hizo ni Miriam Manu, amabaye ameiambia Swahillivilla kuwa anajisikia furaha kukamilisha funga ya Ramadhani na kuweza kusherekea siku hii adhimu kwa Waislamu.
"Najisikia furaha na namshukuru Allah kwa kila kitu alichoniwezesha kuwa nacho, khususan kuniwezesha kufunga na kunifikisha katika siku hii na kusherehekea", alisema msichana huyo ambaye makazi ya ugenini yamemfanya asiweze kuzungumza Kiswahili, na hivyo kuongea nasi kwa Kimombo.
Aliendelea kusema: "Mama yangu alikuwa akiniambia kuwa kufunga kunakufanya ufahamu ni jinsi gani watu masikini na waiokuwa na uwezo wanajihisi wanapokuwa na njaa, na hii inakupa moyo wa kuwasidia watu wengine wenye matatizo na mambo kama hayo"
Miriam aliendelea kusema "Hii ni siku ya furaha, kwani sote tunajumuika pamoja, tunaswali pamoja, tunacheza, kucheka na kula pamoja. Ni siku ya furaha kwani tunapata nafasi ya kukutana na marafiki wa zamani na kupata marafiki wapya, na ni jambo la kusikitisha pale sherehe zinapomalizika tunalazimika kuagana na marafiki zetu.
Itafaa kukumbusha kuwa Sherehe za TAMCO huchukua masaa kadhaa, na kwa hivyo Waislamu hupata fursa ya kuswali Swala za Alasiri, Mgharibi na Isha kwa jamaa katika viwanja hivyo, kama alivyodokeza Miriam.
Naye msichana Sheri Juma hakusita kuelezea furaha yake kwa siku hii yenye umuhimu mkubwa kwa Waislamu.
"Siku ya Iddi ni siku ya furaha kwangu, kwani huamka asubuhi kuonana na familia yangu, kisha tunakwenda kuswali na kumshukuru Mola kwa kila alichonijaalia maishani mwangu, kisha tunakuja hapa kukutana na marafiki". Alisema Sheri kwa sauti na uso wenye bashasha, huku midomo ikiwa tayari kuitafuna mishikaki.
Itakumbukwa kuwa nchini Marekani kumekuweko na matukio ya hapa na pale yenye chuki dhidi ya Waislamu, na kwa hivyo mikusanyiko kama hii ni nafasi ya kuimarisha mshikamano miongoni mwa Waislamu kama anavyotukumbusha msichana Aziza Mattaka:
"Ni jambo la faraja kwetu kukutana katika mjumuiko kama huu kama Jamii ya Waislamu khususan baada ya matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni yenye kuonesha chuki dhidi ya Waislamu, kwa hivyo ni jambo la busara kukutana kama hivi baada ya Mfungo wa Ramdhani, na najisikia faraja baada ya kukamilisha Swaumu yangu na kuja kujumuika na jamaa na marafiki".

No comments: