ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 28, 2017

SIMIYU KUNUFAIKA NA MRADI MKUBWA WA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA KWA UFADHILI WA MFUKO WA MABADILIKO YA TABIANCHI

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora akifungua mkutano wa wadau wa Utekelezaji wa Mradi wa Maji Simuyu. Mradi huo mkubwa uko katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kutekelezwa. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Eng. Emmanuel Kalobelo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Eng. Emmanuel Kalobelo akifunga kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora.
Katibu Mkuu Prof. Faustin Kamuzora (watatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi wanaohusika na utekelezaji wa Mradi wa maji wa Simiyu mara baada ya ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.

Na Lulu Mussa, Dodoma
Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) imepata fedha za kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Mkoa wa Simiyu ambapo fedha za Mradi huo zitapitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora wakati wa kikao kazi kilichojumuisha wadau wanaohusika na utekelezaji wa Mradi wa maji wa Simiyu, mradi unaofadhiliwa na Mfuko wa mabadiliko ya tabianchi ambapo imebainika kuwa utekelezaji wake utaanza mara moja.
Aidha, Prof. Kamuzora amesema kuwa fedha hizo zinapitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani kutokana na sababu kwamba Serikali ya Ujerumani imekua ikifadhili miradi mbalimbali ya maji hapa nchini. “Ili kupata fedha kutoka katika mfuko huu ni lazima zipite kwenye taasisi ambayo imethibitishwa “accredited entity”alisisitiza Profesa Kamuzora.
Prof. Kamuzora amesema kuwa huu ni mradi mkubwa sana na wenye manufaa kwa wakazi wa Simiyu ambapo Mfuko wa Mabadiliko ya tabianchi umetoa kiasi cha 102,700,000 EURO, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) itachangia 25,900,000 EURO na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itagharamia kiasi cha 13,100,000 EURO. Vilevile jamii inayozunguka mradi itachangia kiasi cha 1,500,000EURO, hivyo mradi wote unatarajiwa kugharimu kiasi cha EURO 143,000,000 na utatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Mradi huo pia una lengo la kuimarisha afya za wakazi hao, kuhimiza uzalishaji endelevu na maendeleo ya jamii inayozunguka kwa kuwapatia maji safi na salama kwa miji na vijiji ambapo mradi utapita pamoja na kuhimili mabadiliko ya tabianchi hususan kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu.
Akitoa maelezo ya awali juu ya Mradi huo Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabia Nchi anayeiwakilisha Afrika Bw. Richard Muyungi, amesema kuwa ni mradi mkubwa sana na wa kwanza duniani kupatiwa fedha kupitia mfuko huo ambazo si mkopo. “Ni fedha zisizo za mkopo, ni msaada hivyo katika awamu ya kwanza takriban watu 395,000 katika Wilaya ya Busega, Bariadi na Itilima watanufaika na mradi huo”
Kupatikana kwa mradi huu na utekelezaji wake utasaidia sana changamoto zitokanazo kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ukame uliokithiri na utasaidia kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi katika Wilaya husika.
Kikao cha Wadau  cha kujadili utekelezaji wa Mradi wa maji wa Simiyu, kimeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais  ambao ni Wasimamizi wa Fedha za Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi hapa nchini na wanadhamana ya kuhakikisaha fedha za Mfuko huo zinatumika ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuendana na mipango nchi iliyojiwekea.

No comments: