Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu kifungo cha maisha jela, dereva Furaha Chuga (38) baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kike wa miaka minane.
Chuga ambaye ni mkazi wa Kiwalani, amehukumiwa adhabu hiyo leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, baada kumtia hatiani kwa kosa hilo la kumlawiti mtoto huyo katika bonde lililopo jirani na nyumba yao na kisha kumpatia Sh 1000.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Hassan amesema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka akiwemo, shangazi wa mtoto huyo na daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, aliyemfanyia vipimo.
Hakimu Hassan amesema kuwa amemtia hatiani mshtakiwa huyo kama alivyoshtakiwa na hivyo kumhukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya mshtakiwa huyo.
“Sina sababu yoyote ya kutokuamini ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne akiwemo mhanga wa tukio, hivyo mahakama yangu inakutia hatiani kama ulivyoshtakiwa na kwamba utatumikia kifungo cha maisha jela” amesema Hassan na kuongeza.
Kabla ya kumtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo, kwanza Hakimu Hassan alipitia ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi wa mshtakiwa.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, mtoto huyo amegunduliwa na shangazi yake kuwa alikuwa ameingiliwa na hawezi kutembea vizuri huku akitoka haja kubwa kila wakati.
Kwa mujibu wa ushahidi huo, Chuga alimtuma mtoto huyo kwenda kununua sigara na aliporudi alimpeleka bondeni na kisha kumvua nguo na kumlawiti.
Katika ushahidi wake mtoto huyo aliieleza mahakamani kuwa alitumwa na mshtakiwa kwenda kununua sigara dukani na aliporudi alimpeleka bondeni na kisha kumvua nguo na kutoa uume wake na kuanza kumlawiti huku akimziba mdomo, asipige kelele.
Mtoto huyo aliendelea kueleza kuwa wakati akifanyia kitendo hicho alikuwa anasikia maumivu makali sehemu ya haja kubwa, na kwamba mshtakiwa huyo alikuwa akimpatia Sh 1000 kila alipomlawiti na kumuonya akae kimya asimwambie mtu yoyote.
Binti huyo amesema ameshalawitiwa mara saba lakini alikaa kimya bila kumwambia bibi yake hadi alipogunduliwa na shangazi yake.
Alidai wakati akifanyiwa kitendo hicho alikuwa anasikia maumivu na kwamba fedha hiyo aliyokuwa akipewa alikuwa anaitumia kununulia vitu shuleni.
Kwa upande wa shangazi wa mlalamikaji alidai kuwa amegundua mtoto huyo kuwa na tatizo baada ya kumuona kuwa anashindwa kutembea vizuri huku akitoka maji sehemu ya haja kubwa na kinyesi.
Shangazi huyo alidai kuwa baada ya kuona hivyo, alimvua nguo binti huyo na kuanza kumwangalia ambapo alibaini kuwa binti huyo alikuwa anaingiliwa na alipomuuliza, alimwambia kuwa amelawitiwa na rafiki wa babu yake ambaye ni Chuga.
Katika utetezi uliotolewa mahakamani hapo na Chuga alidai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama mlezi wa mtoto huyo lakini baadae waliachana hivyo tuhuma za kulawiti zimetengenezwa.
Awali, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili wa Serikali Grace Mwanga ameomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizi za kulawiti watoto wadogo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment