ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 23, 2017

KODI YA PANGO LA ARDHI SASA KIDIGITALI

Mtaalamu wa mfumo wa GePG (Government electronic Payment Gateway) kutoka Wizara ya fedha akielezea faida za mfumo kwa watumiaji pamoja na jinsi ya kuutumia katika kutoa huduma bora.
Mafunzo juu ya matumizi ya mfumo wa GePG yakitolewa kwa maofisa wa ofisi za Ardhi Nyanda za Juu Kusini
Wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi pamoja na maofisa kutoka ofisi za Ardhi Nyanda za Juu Kusini wakifuatilia mafunzo kwa umakini
Mtaalamu kutoka Wizara ya Ardhi (aliyesimama nyuma) akitoa msaada jinsi ya kutumia mfumo kwa maofisa wa ofisi za Ardhi Nyanda za Juu Kusini
Mtaalamu kutoka Wizara ya Fedha akionesha mfano wa fomu za benki ya NMB ambazo mwananchi atapaswa kujaza akienda kulipia kodi ya pango la Ardhi katika benki hiyo.

NA: ELIAFILE SOLLA

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekusudia kuboresha huduma zake pamoja kuzisogeza karibu zaidi na wananchi ambao ndio wateja wakubwa wa Sekta hiyo. Hii ni katika kuboresha utoaji huduma na kuongeza ufanisi wa huduma za Ardhi.

Katika kuhakikisha hili linafanikiwa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaanzisha mifumo ambayo itakuwa inatumika kama njia rahisi ya utoaji huduma kwa wananchi. Mifumo yote hiyo ni kwa lengo la kuboresha huduma, kurahisisha huduma na pia kuondoa urasimu ambao ungeweza kujitokeza katika utoaji wa huduma kwa mwananchi.

Mfumo wa GePG (Government electronic Payment Gateway) ni mfumo wa Serikali ambao umetengenezwa kwa lengo la kukusanya na kusimamia mapato ya Serikali. Mfumo huu pia utakuwa unatumiwa na Wizara kuu za Serikali, Taasisi za kifedha, Makampuni ya simu, Serikali za mitaa na Idara zote za Serikali ambazo zina vyanzo vya mapato.

Malipo yote yatakuwa yanalipwa kwa kutumia namba maalumu ya malipo inayojulikana kama “control number” ambayo itamuwezesha mwananchi kulipia katika benki za NMB, CRDB au kwenye Mpesa na Tigo pesa mahali popote.

Mwananchi anaweza kupata makadirio yake ya kodi ya pango la Ardhi kwa kutumia mfumo huu wa GePG. Hii ndiyo maana halisi ya kusema sasa huduma za sekta ya Ardhi zinaboreshwa kwa kuondoa usumbufu wa kutembelea vituo vya makusanyo.

Njia mojawapo ya kupata makadirio ni kwa kutumia tovuti ya Wizara ya Ardhi (www.ardhi.go.tz). Utachagua ‘kadiria kodi ya Ardhi’ na kisha utafuata maelekezo ya namna ya kuingiza taarifa za kiwanja chako. Baada ya kuingiza taarifa sahihi utabonyeza kitufe cha kadiria na hapo utapata taarifa za deni la kodi ya pango la ardhi pamoja na namba ya kulipia inayoanzia 99117…..

Pia unaweza kupata makadirio ya kodi ya pango la ardhi kupitia simu ya mkononi kwa kuingiza menyu kuu ya taifa ambayo ni *152*00# , kisha unachagua namba 4 malipo ya Serikali. Baada ya hapo utachagua namba 2 kadiria kodi ya kiwanja ambapo, utachagua nmba 1 kwa viwanja vya Dar es Salaam au namba 2 kwa viwanja vya mikoa mingine. Utachagua 1 kama unajua namba ya kiwanja au 2 kama unajua Lot ID na hapo hapo utapokea ujumbe wa malipo ukiwa na kumbukumbu namba inayoanzia na namba 991177….. Ukishapokea huo ujumbe utakuwa na uwezo wa kulipia katika beki za CRDB, NMB na kwa Mpesa au Tigo pesa.

Malipo yoyote yakifanyika kupitia simu ya mkoni, mwananchi atapokea uthibitishpo wa malipo ambao ni risiti namba. Nakala ngumu ya risiti (hard copy) inapatikana katika kituo chochote cha makusanyo, mwananchi atapaswa kwenda na uthibitisho wake wa malipo tuu ili kupatiwa nakala ngumu ya stakabadhi.

No comments: