Mashahidi wawili akiwemo Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ofisa wa Polisi, Ramadhan Kingai leo wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi Mfanyabiashara Yusuf Manji alivyopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kupimwa mkojo.
Mbali ya Kingai ambaye ni Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ya dawa za kulevya inayomkabili Manji, Shahidi mwingine ni E.1125 Copro Detective Sospter.
Mashahidi hao walitoa ushahidi wao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Timony Vitalis kueleza kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya ushahidi.
Akiongozwa na Wakili Vitalisi, Shahidi Kingai amedai kuwa February 9, 2017 akiwa Ofisini kwake Central alikuwa na kazi mbalimbali ikiwemo ya kuripotiwa kwa watuhumiwa wa Dawa za kulevya waliotajwa na RC Makonda.
Amedai katika watuhumiwa hao alimpokea Yusuf Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima baada ya kuripoti wenyewe kituoni hapo.
“Baada ya kufika nikiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi wa dawa za kulevya nilielekeza Manji na Gwajima wapelekwe kwa Mkemia Mkuu kupimwa, kwa sababu tuhuma zao ni za dawa za kulevya, ambapo pia walienda kupekuliwa nyumbani mwao”
Shahidi huyo akadai kuwa amri ya kupimwa ilitekelezwa na Detective Copro Sospeter, ambapo baada ya kufanyika uchunguzi akapewa taarifa kwamba Manji anatumia Dawa za kulevya aina ya Benzodiazepines na Gwajima hatumii.
“Nikiwa kama Mpelelezi Mkuu niliichukua ripoti hiyo kisha nilielekeza Manji afunguliwe jalada la kutumia dawa za kulevya ambapo baada ya kufunguliwa lilipelekwa kwa DPP”.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Manji, Hudson Ndusyepo alimuuliza shahidi huyo kwa nini dawa za kulevya (Benzodiazepines) alizozitaja Mkemia Mkuu ni tofauti na zilizotajwa kwenye hati ya Mashtaka (Heroin) ambapo shahidi huyo alijibu hajui na yeye hakuandaa hati ya mashtaka.
Shahidi wa pili, Detective Copro Sospeter akiongozwa na Wakili Vitalis alidai kuwa February 9, 2017 saa 5 asubuhi alikuwa Ofisini na alimpeleka Manji kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuchubguzwa.
Alidai kuwa maelezo ya kumpeleka Manji kwa Mkemja aliyapata kwa Kingai, ambapo alimpeleka kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya.
” Nilimchukua Manji na kumpeleka msalani ili ichukuliwe sampo ya mkojo wake ufanyiwe uchunguzi, ambapo kuna kielelezo cha fomu kuhusu suala hilo na naomba kipokelewe na Mahakama.”
Alieleza kuwa baada ya mtuhumiwa kuchunguzwa alichukua majibu kisha alirejeshwa Polisi na taratibu kufatwa.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hadi August 23, 2017.
No comments:
Post a Comment