MCHEZAJI anayeongoza kwa kupendwa na mashabiki wa Simba, Emmanuel Okwi ametamka kwa mdomo wake kuwa kiungo mpya wa Yanga, Kabamba Tshishimbi ni fundi na anajua kazi yake.
Okwi amesema wazi kuwa kiungo huyo mpya wa watani zao, anajua soka na kumvulia kofia kwa namna alivyokipiga katika mechi ya Ngao ya Jamii juzi Jumatano pale Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Straika huyo aliyewahi kucheza Yanga, alisema Tshishimbi anacheza soka la kazi, ushindani pamoja na kuburudisha na kwamba kama hiyo juzi alishuka uwanjani akiwa hayupo fiti kwa asilimia zote, hajui akiwa fiti atakuwaje kwa mpira mwingi aliowapigia Taifa.
Katika mechi hiyo ambayo Yanga ililala kwa penalti 5-4 baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana, kiwango cha Mkongomani huyo kimemfanya Okwi aliyewahi kuifunga Yanga mara tatu kuthubutu kutamka neno kutoka moyoni ambalo hata kocha wake, Joseph Omog alilikubali.
“Tshishimbi ana uwezo mkubwa, ameweza kucheza maeneo mengi, anajituma kuhakikisha timu yake inakuwa na mafanikio. Uchezaji wa aina yake ni wa mchezaji mwenye kuona mbali, hivyo wamepata mtu atakayewasaidia kwenye ligi na mashindano mengine,” alisema Okwi.
Mbali na Okwi, kiungo fundi wa kuchezea mpira, Haruna Niyonzima, naye alimzungumzia Tshishimbi na kumpa sifa kwamba Yanga wamepata mtu ambaye walimtafuta kwa muda mrefu.
“Nashukuru kwa kupata ushindi katika mechi yangu ya kwanza, ila nitoe pongezi kwa kiungo mpya wa Yanga Tshishimbi, alikuwa kikwazo kikubwa kwetu na pengine ndio alifanya tushindwe kupata ushindi ndani ya dakika tisini,” alisema.
Kiungo mwingine wa Simba, Mghana James Kotei naye alifunguka na kusema kuwa katika usajili ambao Yanga wameufanya msimu huu, basi Mkongomani huyo ndiye fundi na atawabeba katika mechi nyingi zilizopo mbele yao.
KIGOGO SIMBA AMZUNGUMZIA
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulliy, alisema Yanga ilikuwa ife katika mchezo huo, lakini uchawi wao ulibebwa na Tshishimbi ambaye kila alipogusa mpira uwanja mzima ulizizima.
“Niseme ukweli pengine ndiyo usajili mkubwa kwa Yanga ni mtu ambaye binafsi nimeridhika na kiwango chake. Huyu ni kiungo wa kweli, anajua majukumu yake amewasaidia sana Yanga katika kiungo chao, lakini naona kama bado hana mazoezi ya kutosha,”alisema Tulliy
LWANDAMINA HUYU
Wakati Tulliy na Wanasimba wengine wakimzungumzia kiungo huyo mwenye miaka 27, kocha wa Yanga, George Lwandamina amesema Mkongomani huyo alionyesha thamani ya kwamba kwanini viongozi wa Yanga walipania kumsajili, lakini akasema bado kuna mengi yatakuja kutoka kwake.
Lwandamina alisema alimtaka Tshishimbi kucheza kwa asilimia 70 tu katika mchezo huo akihofia anaweza kuumia kutokana na kukosa mazoezi mazito, lakini ana imani wana Yanga watafurahia zaidi utamu wa kiungo huyo.
“Huyu ni mchezaji bora alikuwa ni kitu muhimu katika timu yetu nafikiri amewapa faraja viongozi wa Yanga na mashabiki wao katika mchezo huu,” alisema Lwandamina.
“Tulichelewa kumpata nafikiri angefika mapema wakati tunaanza maandalizi angekuwa bora zaidi lakini alichekewa ndiyo maana nilimtaka asicheze kwa kiwango kikubwa sana angeweza kuumia”
IMEANDIKWA NA OLIPA ASSA, KHATIMU NAHEKA NA THOBIAS SEBASTIAN
No comments:
Post a Comment