ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 25, 2017

Wakili ashauri kesi ya Kitilya ifutwe

Wakili Majura Magafu ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuulazimisha upande wa mashtaka kuifuta kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), Harry Msamire Kitilya na wenzake ama waiondoe wenyewe kwa uungwana wao.
Ombi hilo, aliliwasilisha leo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, mara baada ya Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa kudai upelelezi haujakamilika na kwamba bado hawajapokea awamu ya pili ya nyaraka kutoka Uingereza.
Baada ya kutolewa maelezo hayo, Magafu alisema umefika wakati maelekezo yanayotolewa na mahakama yaheshimiwe na kuheshimiwa.
Magafu alidai kuwa mahakama haifungwi mikono kuulazimisha upande wa mashtaka kuifuta kesi hiyo ama waifute wenyewe kwa uungwana wao.
Kwa sababu washtakiwa hao awali walikuwa na dhamana na walikuwa wakiripoti kila walipohitajika Takukuru.
"Nadhani utaratibu huo unaweza kutumika na upande wa mashtaka watakapokamilisha upelelezi wawalete mahakamani,"alieleza Magafu.
Alibainisha kuwa tangu upande wa mashtaka useme umekwisha pokea awamu ya kwanza ya nyaraka toka Uingereza, ni miezi sasa na imekuwa hadithi kuwa vya awamu ya pili bado havijafika. Hivyo aliiomba mahakama kutumia mamlaka yake kuifuta.
Wakili Msigwa alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo unavuka mipaka na kwamba si kuwa Jamhuri imelala, inahangaika kufanya mawasiliano na upande zote.
Hakimu Mkeha alimueleza Magafu kuwa anafahamu mahakama haina mamlaka kwenye kesi hiyo na akaiahirisha hadi Septemba 9, 2017.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Graham Solomon. Washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Agosti, 17, 2016.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

No comments: