Advertisements

Wednesday, August 9, 2017

WAZIRI MKUU APOKEA MSAADA WA MAGARI KUTOKA KAMPUNI YA FOTON

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea Funguo za Magari matatu yenye thamani ya Dola za kimarekani 99,700 ambayo amekabidhiwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Foton International kutoka China Bwana Zhao Xiano Kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo nchini Tanzania, wanaoshuhudia kutoka kushoto  ni Meneja masoko wa kampuni ya Simba Motors Taanzania Bibi Ifigenia Salazar na kutoka kulia ni Afisa masoko wa Foton International, Bwana Fan Liang. Makabidhiano hayo yamefanyika leo ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es salaam. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia moja ya magari aliyokabidhiwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Foton International kutoka China Bwana Zhao Xiano Kwa ajili ya kusaidia shughuli zamaendeleo nchini Tanzania Makabidhiano hayo yamefanyika leo ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es salaam.  Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa magari matatu yenye thamani ya Dola za Marekani 99,700 kutoka Kampuni ya Foton International Trade Co. Ltd ya nchini China.

Amepokea msaada huo leo (Jumatano, Agosti 9, 2017) jijini Dar es Salaam, ambapo amesema magari hayo yatatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii nchini. Magari hayo ni Sauvana SUV moja na Tunland Double cabin mbili.

“Nashukuru kwa msaada huu wa magari uliotolewa na Kampuni ya Foton kwa Serikali yetu. Magari haya yanaweza kutumika katika Hospitali za wilaya kwa ajili ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kutolea elimu mbalimbali kwa umma.”

Pia, Waziri Mkuu ameikaribisha Kampuni hiyo kuja nchini kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari. Amesema mbali na utulivu wa kisiasa uliopo Tanzania, pia kuna sera na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw. Zhao Xiao amesema wametoa msaada huo wa magari kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Tanzania hususan maeneo ya vijijini.

Bw. Xiao amesema Kampuni ya Foton inatengeneza magari 700,000 kwa mwaka, ambayo  yanauzwa katika nchi 125 duniani. Amesea ifikapo mwaka 2020 wanatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia magari milioni 1.4 kwa mwaka.

Kuhusu suala la kuja kuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari nchini, Bw. Xiao amesema wanampango wa kuwekeza nchini kwa kuwa  kuna fursa nzuri za uwekezaji na uhakika wa masoko katika nchi zingine za Afrika Mashariki.
                                                   
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 9, 2017

1 comment:

Tumaini Geofrey Temu said...

Baadaya kupokea msaada wa utaalamu wa kuunda magari yunapokea msaada wa kununua spare parts