ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 26, 2017

WAZIRI MWIGULU NCHEMBA AAGIZA WAENDESHA BODABODA WOTE KUNUNUA KOFIA NGUMU NDANI YA MWEZI MMOJA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akizungumza na waendesha bodaboda na baiskeli 'daladala' leo mjini Shinyanga-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ameagiza waendesha bodaboda wote nchini kuhakikisha kuwa wanakuwa na kofia ngumu ‘Helmet’ ndani ya mwezi mmoja baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa.

Mheshimiwa Nchemba ametoa agizo hilo leo Jumamosi Agosti 26,2017 mjini Shinyanga wakati akizungumza na waendesha bodaboda na baiskeli 'daladala' zaidi ya 300 wanaofanya shughuli zao katika manispaa ya Shinyanga.

Alisema kosa la kutovaa kofia ngumu litawahusu wamiliki wa bodaboda,waendesha bodaboda pamoja na abiria ambao kwa pamoja watawajibika kila mmoja kwa nafasi yake.

“Hili litafsiriwe vizuri kila eneo katika nchi yetu,kwanza kabisa kama mmiliki hajaweka kofia mbili,bodaboda ikikutwa haina kofia mbili,tatizo lile linaenda kwa mmiliki,pili kama mwendesha bodaboda amepewa kofia mbili halafu akaamua kuziacha huyo ana kosa”,alieleza.

“Tatu, kama mwendesha bodaboda ana kofia zote mbili lakini mbebwaji/abiria hataki kuvaa kofia,mwacheni mwenye pikipiki aende na pikipiki yake,huyo mbebwaji atakuwa na kosa la kuhatarisha maisha yake ili kila mmoja atimize wajibu wake”,aliongeza Nchemba.

Mheshimiwa Nchemba pia alisisitiza umuhimu wa abiria wanaopanda katika bodaboda kukaa mkao wa kiume ili kuepusha ajali za barabarani.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amepiga marufuku ukamataji wa bodaboda unaofanywa na askari polisi kwa kufukuzana na waendesha bodaboda kwani inachangia kutokea kwa ajali.

“Tumeelekeza ukamataji wa kistaarabu,ukamataji huu wa kistaarabu ufanyike kwa nyinyi mtimize wajibu ili kuwe na tofauti ya aliyekosa na ambaye hajakosa,na sisi askari lazima tutofautishe aliyekosa na ambaye hajakosa ili tuwe marafiki na hawa watu”,alisema Nchemba.

“Tunafanya haya kwa ajili ya maisha yenu,hatuna upendo zaidi ya kuokoa maisha yenu,hatutaki watu wapoteze maisha kwa sababu ya uzembe wa waendesha bodaboda ama abiria”,aliongeza Nchemba.

Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule alisema kikao hicho cha Waziri wa Mambo ya Ndani ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya jeshi la polisi katika zoezi la utoaji elimu kuhusu masuala ya usalama barabarani.

“Hivi karibuni katika mkutano wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga,uliolenga kusikiliza kero za wananchi,kuna mambo yaliibuliwa ikiwemo la waendesha bodaboda kutofahamu matumizi mazuri ya Mzunguko wa barabara ‘Round About’ hivyo tunatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Round about”,alieleza Kamanda Haule.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack,alisema ajali za barabarani zimepungua kutokana na waendesha bodaboda kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini,Mheshimiwa Stephen Masele (CCM) aliwataka waendesha bodaboda kufuata sheria za usalama barabarani na askari polisi waache kutumia nguvu kubwa kukabiliana na waendesha bodaboda.

MSIKILIZE HAPA WAZIRI MWIGULU NCHEMBA AKITOA MAAGIZO LEO SHINYANGA
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akizungumza na waendesha bodaboda na baiskeli 'daladala' leo mjini Shinyanga.Kulia ni Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule.Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack.
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akiwasisitiza waendesha bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akizungumza.
Waendesha bodaboda na baiskeli mjini Shinyanga wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Ndani,Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akizungumza na waendesha bodaboda na baiskeli.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akizungumza wakati wa kikao hicho.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule akizungumza wakati wa kikao hicho.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Simon Haule akieleza namna jeshi la polisi linafanya ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga,Anthony Masanzu akisisitiza jambo wakati kikao hicho.
Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini,Mheshimiwa Stephen Masele (CCM) akizungumza katika kikao hicho.
Kikao kinaendelea.
Mmoja wa waendesha akiuliza swali kwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mheshimiwa Josephine Matiro akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho.
Mkazi wa Shinyanga Mjini akieleza shida yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani,Mheshimiwa Mwigulu Nchemba baada ya kikao kufungwa.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

No comments: