ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 26, 2017

Inspekta aeleza jinsi Manji alivyoumwa gerezani

Mfanyabiashara Yussuf Manji akizungumza na
By Tausi Ally, Mwananchi

Daktari Mfawidhi wa Gereza la Keko, Inspekta Eliud Mwakawanga ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi maisha ya mfanyabiashara Yusufu Manji yalivyokuwa gerezani kwamba alikuwa akitumia vidonge kati ya 25 mpaka 30 kwa siku.

Ameeleza kuwa walikuwa wakipatia dawa hizo alipokuwa akisikia aumivu hasa ya mgongo na kwamba kuna kipindi alikuwa anaamka akiwa na hali ya kutetemeka au kuchanganyikiwa.
Pia ameeleza kuna wakati Manji alikuwa anaamka anashindwa hata kutembea na wakati mwingine alikuwa akitumia mkanda kufunga mgongo.

Shahidi huyo wa sita wa upande wa mashtaka ametoa ushahidi huo leo Jumanne katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin inayomkabili Manji.

Ameeleza kuwa Julai 6, 2017 walimpokea Manji akitokea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha Moyo cha JKCI ambapo waliambiwa ni mshtakiwa lakini ni mgonjwa.

“Nilienda kumuona, tukazungumza naye na tulikaa naye gerezani hadi alipokuja kuachiwa,”
"Tangu nimempokea hali yake kiafya haikuwa nzuri na alikuwa mtu anayetumia dawa wakati wote na alikuja na dawa zake za aina sita kutoka Muhimbili ambazo alikuwa akizitumia, pia kulingana na hali yake na mazingira anayokuwa anajisikia, tulikuwa tukimpatia dawa gerezani mbali na hizo."
Ameeleza kuwa utaratibu wa kuwapatia dawa mahabusu na wafungwa huwa wanakaa nazo wao wataalam na wanawapa kutokana na maelezo ya daktari yaliyopo kwenye cheti ambapo Manji kuna dawa alikuwa anakunywa asubuhi na jioni na nyingine kulingana na hali yake ya siku hiyo.
Shahidi huyo ameeleza kuwa wao huwa hawatoi dawa za kulevya kwa mgonjwa ila wanatoa dawa.
Alisema hivyo baada ya kuulizwa na Wakili Hajra Mungula kuwa dawa walizompatia Manji zinahusiana vipi na dawa za kulevya.

"Sijachunguza sana kuona zina uhusiano gani na dawa za kulevya,” ameeleza na kusisitiza wao hawatoi dawa za kulevya kwa mgonjwa wanatoa dawa.
Kesi hiyo bado inaendelea mahakamani hivi sasa kwa taarifa zaidi soma gazeti la Mwananchi

No comments: