Advertisements

Tuesday, September 26, 2017

Mambosasa ataka uthibitisho miili iliyookotwa Coco Beach

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro
Dar es Salaam. Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema hajapelekewa uthibitisho kuhusiana na maiti za wanaume watatu waliokutwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach.

Amesema kwamba iwapo atapelekewa udhibitisho huo ni lazima atatolea ufafanuzi suala hilo kiundani zaidi.

Maiti za watu hao zilikutwa juzi Septemba 24 ambapo mbili zilifungwa kwenye viroba huku nyingine zikiwa ikiwa imekutwa na jiwe kubwa lililofungwa na kamba.

“Sijaletewa ‘fact’ nikiletewa nitalitolea ufafanuzi,”amesema Mambosasa.

Wafanyabiashara wa mihogo wa eneo hilo wamesema wakiwa kwenye biashara zao asubuhi ghafla waliona maiti moja ikielea karibu na miti aina ya mikoko ikiwa na jiwe lililofungwa kifuani huku mikono yake ikifungwa na kamba.

Mmoja wa wafanyabiashara, Aziza Ally amesema baada ya kuona maiti hiyo walitoa taarifa polisi ambapo walifika saa 4 asubuhi na kuichukua kwenye gari lao.

Amesema ilipofika saa 8 mchana waliona maiti mbili kila moja ikiwa kwenye kiroba zikielea ndipo mmoja wao alipoamua kutoa taarifa polisi baadaye zikachukuliwa.

"Polisi walipokuja kuchukua hizi maiti hakuna hata mtu mmoja aliyeruhusiwa kusogelea na kupiga picha tulishangaa sana kuona ulinzi mkali tofauti na siku zote na aliyebainika amepiga alipokonywa simu yake," amesema Ally.

Mfanyabiashara mwingine Issa Isaya amesema cha kushangaza maiti zinazookotwa ni za kiume pekee.

Amesema wanaishi kwa wasiwasi kwasababu kila wiki wanakuta maiti zikiwa zinaelea kwenye maeneo hayo.

MWANANCHI

No comments: