Boti Jeupe lililonaswa na kikosi maalumu cha kuzuia uhalifu cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) juzi wakati wahalifu wakijiandaa kutoboa bomba na kuiba mafuta kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi. Wahalifu walifanikiwa kutokomea kusikojulikana baada ya kujitosa baharini, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari-TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kuhusu mafuta yanavyopakuliwa kutoka kwenye meli, alipotembelea bandarini hapo ili kupata maelezo kuhusu mchakato wa kupata mita mpya za kupimia mafuta (Flow Meters), Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko (kushoto) akimuonesha Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), namna maharamia wa mafuta walivyoharibu miundombinu ya bomba la mafuta baharini, baada ya kufanikiwa kukamata boti moja na vifaa vyake lililokuwa likitumiwa na wahalifu hao kuiba mafuta.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), akiwapongeza askari wa doria waliofanikisha kukamata boti moja pamoja na vifaa vyake muhimu ikiwemo injini baada ya kuwadhibiti maharamia waliotaka kutoboa bomba na kuiba mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mmoja wa maafisa wa TPA walioongoza zoezi la kupambana na wahalifu wanaoiba mafuta kwenye bomba la mafuta akionesha vilipuzi vilivyokamatwa vilivyokuwa vitumiwe na wahalifu waliokuwa wakijaribu kuiba mafuta kwenye bomba la mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiangalia baadhi ya vifaa ikiwemo injini ya boti, vilivyokamatwa baada ya wahalifu kukurupushwa baharini wakijaribu kuiba mafuta kwa kutoboa bomba baharini.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia)na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko (kulia) na wengine, walipotembela Bandari ya Dar es Salaam, kitengo cha Mafuta, kukagua flow meters na tukio la kukamatwa kwa boti lililokuwa likitumika kuhujumu bomba la mafuta.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati), akiwa juu ya mitambo ya kupitisha mafuta kutoka kwenye Meli alipokuwa akipata maelezo ya namna Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, inavyodhibiti mafuta ili Serikali ipate kodi yake stahiki.
Kaimu Kamisha na Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Elijah Mwandumbya, akitoa maelezo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), kuhusu hatua zilizochukuliwa kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali upande wa mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, akitoa maelezo walipokuwa wakiagana na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).Katika ziara hiyo Waziri Mpango amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania na Mamlaka ya Mpato katika kudhibiti ukwepaji kodi.
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, ameiomba Serikali kuipatia Mamlaka yake vitendeakazi muhimu ili kukabiliana na vitendo vya uharamia wa bomba la mafuta katika bahari ya Hindi.
Mhandisi Kakoko ametoa maombi hayo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyetembelea bandari hiyo upande wa mafuta na kuelezwa kuhusu tukio lililotokea juzi ambapo TPA wamekamata boti moja lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuiba mafuta kutoka kwenye bomba, baharini.
Katika tukio hilo watu wasio fahamika, wakiwa na mabomu na baadhi ya vilipuzi, walilitelekeza boti lao na kutoweka kusikojulikana kwa kupigambizi baharini baada ya walinzi wa doria kuwakurupusha kwa kurusha risasi hewani.
“Tunaomba tupatiwe vitendeakazi kwa ajili ya kikosi chetu kinachofanyakazi kubwa ya kupambana na uhalifu mbalimbali bandarini hasa magari ili kukiwezesha kikosi hicho kufanyakazi yake kwa ufanisi” alieleza Bw. Kakoko
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameahidi kuipatia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari vitendeakazi ambavyo viko ndani ya uwezo wake kama Waziri ili kuongeza udhibiti wa eneo la maji ya bahari lenye bomba la mafuta.
“Ninawapongenza sana kwa kufanikisha kuwadhibiti maharamia hao ambao wamekuwa wakitumika kuharibu miundombinu ya bomba na mafuta na kuharibu mita za kupimia mafuta, nawaahidi kuwatimizia maombi yenu ya vifaa ambavyo viko ndani ya uwezo wangu” alisema Dkt Mpango’
Alisema kuwa vitendo vinavyofanywa na wahalifu hao vinakwamisha juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu yake na kusabisha hasara kwa wenye mafuta na kuikosesha Serikali mapato kutokana na vitendo hivyo vya kutoboa bomba na kuiba mafuta.
Mbali na kushuhudia boti lililokamatwa pamoja na vifaa vyake ikiwemo injini na magaloni ya mafuta, Dkt, Mpango alipewa maelezo kuhusu mchakato unaoendelea wa kufunga mita mpya za kupimia mafuta (flow meters).
Mhandisi Kakoko ameeleza kuwa mchakato unaendelea vizuri na kwamba huenda ukakamilika mapema mwakani hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali bandarini hapo.
No comments:
Post a Comment