BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Spika wake Job Ndugai limetoa ripoti maalum kuhusu tukio la kushambuliwa kwa kupigwa risasi Mbunge wa Singida Masgariki, Tundu Antipas Lissu (Chadema) na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake jana mchana.
“Jana mchana baada ya bunge kusitishwa, Lissu aliekea nyumbani kwake Area D, eneo la Site Three, kabla hajashuka kwenye gari watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari aina ya Nisani ambalo namba zake hazikutambulika, walianza kumshambulia kwa risasi.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Kamanda wa Polisi Dodoma, Gilles Muroto, risasi zilizotumika ni kati ya 28 mpaka risasi 32. Risasi kadhaa zilimpata kwenye mwilini, mkononi risasi moja, miguuni risasi mbili na tumboni risasi mbili, kwa hiyo jumla risasi tano zilimjeruhi. Baada ya tukio watu hao walikimbia.
“Lissu alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika kwa kuwa wanaishi jirani. Alipofikishwa aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji kuzuia damu kuendelea kuvuja, ambapo Katibu MKuu wa Wizara ya Afya aliongoza upasuaji huo kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulikuwa umeagiza ndege kwa ajili ya kumchukua mgonjwa kumpeleka Muhimbili. Lakini familia na Mwenyekiti Mbowe, walishauri apelekwe Aga-Khan, Kenya. Walioambatana na mgonjwa ni mke wa Lissu, Mbowe, Daktari Bingwa wa Mkoa wa Dodoma.
“Jeshi la Polisi limeahidi kuwasaka walioshiriki kumjeruhi Lissu na taarifa itatolewa baada ya uchunguzi kufanyika.
“Serikali yetu ina mkataba na Hospitali ya Apollo India na ndiyo channel yetu sote. Kwa nini mwenzetu alipelekwa Nairobi? Hii ni kwa sababu familia iliomba apelekwe huko. Si kwamba hawaamini madaktari wetu. Tulizungumza na familia na Mbowe, wakasema wanawapongeza madaktari wote waliojitahidi kumpa huduma ya kwanza Dodoma, lakini wangejisikia vizuri zaidi iwapo wangeruhusiwa kuchagua hospitali ya kwenda kumtibia. Hivyo tuliona ni jambo jema kwa vile familia imependekeza,” alisema Ndugai.
“Tuendelee kumuombea mbunge mwenzetu kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupona haraka, tutaendelea kupokea taarifa za maendeleo yake Nairobi na tutawajulisha” alimalizia.
Ndugai amewataka wabunge kutoa nusu ya posho zao za leo kwa ajili ya kuchangia matibabu ya mbunge huyo.
No comments:
Post a Comment