ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 21, 2017

THE DESK & CHAIR YAWAPIGA JEKI WATOTO 50 GHARAMA ZA MATIBABU

 Meneja wa kituo cha Nitetee Foundation, Johaness Emmanuel akipokea hundi ya sh. 1,260,000 za malipo ya mchango wa uanachama wa bima ya afya kwa watoto 25 wa kituo hicho kutoka kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, kulia mwenye kinasa sauti ni Mwenyekiti wa Taasisi ya The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania Sibtain Meghjee ambayo imetoa fedha hizo kwa kituo hicho na Karibu Foundation.Kulia mwenye shati ya draft ni Meneja Matekelezo wa NHIF Mkoa wa Mwanza Calistus Mpangala. Picha ya Baltazar Mashaka.
 Afisa Matekelezo wa Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) Mkoa wa Mwanza, Castus Mpangala akitoa ufafanuzi wa huduma zinazotolewa na mfuko huo kwa wananchi waliohudhuria semina ya bima ya afya iliyoandaliwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania ili kuwahamasisha  kujiunga na mfuko huo kwa ajili ya kupata matibabu kwa gharama nafuu. Semina hiyo ilifanyika jijini Mwanza.
 Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella mwenye kofia akiwa ameshika moja ya mashuka yaliyotolewa msaada na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) Mkoa wa Mwanza kwa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe. Wa tatu kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dk.Leonard Subi, Meneja wa mfuko huo mkoani Mwanza Dk. Mohamed Kilolile wanne kulia na  kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Uekerewe Estomiah Chang'a.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (mwenye kofia) hivi karibuni akinunua samaki aina ya Furu kutoka kwa akinamama wachuuzi wa samaki katika Soko la Kakukulu lililopo wilayani Ukerewe. Mkuu huyo wa Mkoa alikuwa wilayani humo kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Picha na Baltazar Mashaka.

NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
TAASISI ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) imekabidhi hundi mbili zenye thamani ya zaidi sh. 2.5 kwa vituo vya Karibu Foundation na Nitetee Foundation ili kuwawezesha  watoto 50 wanaolelewa kwenye vituo hivyo kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF).
Akizungumza jana baada ya kukabidhi hundi hizo Mwenyekiti wa TD & CF Sibtain Meghjee alisema fedha hizo zitatumika kugharamia matibabu ya watoto hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“ Watoto wanaolelewa kwenye vituo vya Nitetee Foundation na Karibu Foundation,  wengi wao wanatoka kwenye familia duni na wanaishi katika mazingira magumu.Tumeona tuwasaidie kwa kuwakinga na magonjwa kwa kuwalipia mchango wa uanachama wa Bima ya Afya wa sh. 54,000 utakaomuwezesha mtoto kutibiwa kwa mwaka mzima ambapo kila kituo kimepewa sh. 1, 260,000 kwa ajili ya watoto 25 ambao wamesajiliwa tayari, ”alisema.
Meghjee alisema kuwa mbali na vituo hivyo taasisi Bilal Muslim Mission of Tanzania pia itapewa msaada huo wa fedha sh. 1,260,000 kwa watu 50 wasio na uwezo ili wajiuge  na mfuko wa NHIF lakini pia The Deskk & Chair nayo itawafadhili watu 50 kwa kuwalipia gharama matibabu kwenye mfuko huo.
Hata hivyo, alivishauri vyombo vya habari viteo fursa kwa kutangaza mambo mazuri ya heri kwenye kurasa za mbele za magazeti badala ya kuwalisha sumu wasomaji inayotokana na habari za migororo ambazo huchukua nafasi kubwa kwenye kurasa za mbele za magazeti.
“ Mkituletea changamoto za wananchi tukazitatua kunairahisishia serikali kuwafikia na itasaidia kuondoa hofu iliyopo baina ya serikali na wananchi dhidi ya Uislamu maana sisi tunaamini uovu hauna nafasi kwa dini yoyote.Niombe magazeti mambo mema na mazuri yatangazwe kwenye kurasa za mbele badala ya mambo mabaya na ya migogoro tu,”alishauri Meghjee.    
Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo Meneja wa Nitetee Foundation Johaness Emmanuel alisema dhana yao ni kuendelea kuielimisha jamii katika ngazi ya familia ili kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili kuwe na jamii ya watu salama na Tanzania salama isiyo na vitendo vya ukatili.
“Ipo dhana kuwa wamiliki wa vituo vya kulea watoto wanajinufaisha kupitia vituo hivyo na vipo kwa maslahi binafsi badala ya watoto.Dhana hiyo ni potofu na ndio maana tunapambana kwa kuelimishaa jamii kupitia vipeperushi, magazeti na vipindi vya televiesheni ili tuwe na jamii ya watu salama bila ukatili,”alisema Emmanuel.
Kwa upande wake, Asumpta Ngatunga wa Karibu Foundation alieleza kuwa ili kupunguza na kutokomeza ukatili  wana mikakati ya kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwenye jamii ili kuoinga vitendo hivyo.
Aidha, Meneja Matekelezo wa NHIF Mkoa wa Mwanza Calistus Mpangala asilimia 31 ya Watanzania wamejiunga na mfuko huo ingawa kuna changamoto za baadhi ya watoa huduma kutowahudumia vizuri wanachama wa mfuko huo.
Alisema NHIF iko mbioni kuajiri wataalamu watakaokuwa wakiratibu huduma zinazotolewa kwenye baadhi ya vituo na hospitali zinazowahudumia wanachama wa mfuko huo na kuhakikisha zinatoa huduma nzuri ili kuondoa malalamiko. 
Mpangala aliongeza kuwa NHIF imeingia mkataba na watoa huduma mbalimbali ambao malipoya madai yao hulipwa ndani ya siku 60 na hivyo lipo tatizo kwa baadhi yao kuchelewesha madai yao ili yahakikiwe kabla ya malipo kufanyika na hao ndiyo wanaotoa huduma mbaya kwa wanachama wa mfuko.

No comments: