Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe Gambo akizungumza na wadau waliohudhuria shughuli ya kumkabidhi bendera ya Taifa kijana Edgar Tarimo anayekwenda nchini Afrika kusini kushiriki mashindano ya wajasiriamali
Katika picha Kutoka kushoto ni mratibu wa tuzo Anzisha TPSF bi. Jane Gonsalves,akifuatiwa na mama mzazi wa Edgar, katikati ni kijana Edgar Tarimo, Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na mwisho ni Mkurugenzi wa taasisi ya sekta binafsi Tanzania Bwana Godfrey Simbeye.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo amekabidhi bendera ya Taifa kwa kijana Edgar Edmund Tairo kwenda nchini Afrika Kusini kuwania tuzo (tuzo hiyo inajulikana kama Anzisha Prize Award) za wajasiriamali vijana barani Afrika.
Katika makabidhiano hayo ambayo kijana Edgar aliambatana na mama yake pamoja na mwalimu wake Mhe Gambo amemtakia kila la kheri kijana huyo katika kufanikisha ndoto zake ili kuuletea heshima mkoa wake na taifa kwa ujumla.
"Ni matumaini yetu kama watanzania tutamwombea kijana huyu aweze kufanikiwa huko aendako ili aweze kuuletea sifa mkoa wetu na taifa kwa ujumla kwani wazo lake hili likichukuliwa kwa uzito mkubwa litakua na tija katika Tanzania ya viwanda tunayoitamani kwa sasa" alisema Gambo.
Mshiriki huyu ni kati ya washiriki wawili wadogo kuliko washiriki wengine kutoka nchi kumi na tatu za Afrika zilizoingia kwenye fainali ya tuzo hizi kama inavyoonyesha Tanzania.
Kijana Edgar Edmund anatarajia kuwasilisha wazo lake la biashara la kutengeneza vigae vya sakafu (paving blocks) kwa kutumia takataka za chupa za plastiki.
Tuzo hii ilianzishwa na African Leadership Academy kwa lengi la kuwawezesha wajasiriamali vijana ambao wana mawazo ya ubunifu yenye kengi la kusaidia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi barani Afrika.
Kwa hapa nchini TPSF ndio taasisi inayosimamia mchakato wa awali wa upatikanaji wa vijana watakaoshindanishwa kuwania tuzo hiyo ambayo inalenga wajasiriamali vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 22 ambao tayari wanamiliki biashara na wangependa kupanua biashara zao lakini hawana mtaji.
Kila mwaka washindi 12 hupata nafasi ya kushiriki mafunzo ya wiki mbili ya ujasiramali katika chuo cha African Leadership Academy ambapo watagawana fedha taslim kiasi cha dola za kimarekani 100,000 ambapi kati ya hizo mshindi wa kwanza atajinyakulia dola 25,000, mshindi wa pili dola 15,000 na mshindi wa tatu dola 12,000 ili kukuza biashara zao.
No comments:
Post a Comment