Mkoa wa Shinyanga umeungana na mataifa mbalimbali duniani kuadhimisha ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 11 mwezi Oktoba.
Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike katika mkoa wa Shinyanga yamefanyika katika kata ya Iselamagazi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.
Sherehe za maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa kike yamehudhuriwa na watoto kutoka maeneo na shule mbalimbali mkoani Shinyanga,viongozi wa serikali na vyama vya siasa,wananchi na mashirika na taasisi zisizokuwa za kiserikali likiwemo shirika la kimataifa la Save the Children.
Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ya “Tokomeza Mimba za utotoni,Tufikie uchumi wa viwanda”.
Akitoa hotuba kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro alisema mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa mimba za utotoni nchini hivyo jitihada mbalimbali zinahitajika kuhakikisha mimba za utotoni zinatokomezwa mkoani humo.
“Ili tufikie uchumi wa viwanda tunahitaji kutokomeza mimba za utotoni ambazo zinachangiwa pia na ndoa za utotoni,ni wajibu wetu serikali,wazazi na wadau wote yakiwemo mashirika na taasisi zinazohusika na masuala ya haki za watoto kuweka nguvu pamoja ili kukomesha vitendo hivi”,alieleza Matiro.
Aidha aliwanyoshea vidole baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakishirikiana na wanaume wanaowapa mimba watoto kwa kumaliza kesi kimya kimya huku wengine wakidiriki kuozesha watoto.
Matiro alitumia fursa hiyo kuliagiza jeshi la jadi sungusungu kuwashughulikia watu wanaowapa mimba watoto huku akitaka elimu zaidi kuendelea kutolewa katika jamii kuhusu haki za watoto.
Matiro pia aliwasisitiza wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao kike na kuwaeleza madhara ya kujiingiza katika mambo ya mapenzi wangali wadogo badala ya kuwaonea aibu huku akiwataka watoto kutokubali kudanganywa na waume ili kuepuka mimba za utotoni.
Naye Meneja wa Shirika la Kimataifa la Save the Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima alisema vitendo vya mimba na ndoa za utotoni litapungua endapo kesi zinazohusu masuala ya watoto zitachukua muda mfupi kumalizika.
“Bado tuna tatizo la mifumo ya utoaji haki,matukio ya ukiukaji wa haki za watoto yanapotokea,mara nyingi vyombo vya dola ikiwemo polisi wamekuwa wakitumia muda mrefu kufanya uchunguzi,hali hii inatoa mwanya kwa wahalifu kuwapa hongo wazazi watoto kisha kumaliza kesi kienyeji na haki ya mtoto kupotea”,alieleza Malima.
Hata hivyo Malima alishauri kuanzishwa mfumo maalumu kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za watoto utakaosimamiwa na serikali kwa kuyahusisha mashirika na taasisi zinazohusika na masuala ya watoto ili jamii iweze kuondokana na mila potofu zinazogandamiza haki za watoto.
Kwa upande wake,Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga,Azza Hilal aliwataka akina mama kuwa mstari katika kuhakikisha watoto wanaenda shule na kukataa watoto wao kuozeshwa kwa tamaa ya mali huku akiwasisitiza watoto kusoma kwa bidii na kutokubali kurubuniwa kuacha masomo ama kuambiwa wafanye vibaya katika mitihani yao ili wakifeli waolewe.
Akisoma risala kwa niaba ya watoto wa kike mkoa wa Shinyanga,Rosemary Richard kutoka shule ya msingi Iselamagazi alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili watoto ni jamii kuwa na uelewa mdogo kuhusu haki za watoto.
Alizitaja changamoto zingine kuwa ni mila potofu,watoto kutoshirikishwa katika maamuzi na kutoa mawazo katika familia,kubakwa,kupewa mimbana kukatishwa masomo ili wawe chanzo cha mapato wanapoolewa.
Aliiomba serikali na wadau kutoa elimu kuhusu haki na sera za mtoto huku akiitaka serikali kuwachukulia hatua kali watu wanaowafanyia ukatili watoto lakini pia akaomba katika kila shule kutenga vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi.
Mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike,mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack,akitoa hotuba katika kata ya Iselamagazi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini Oktoba 11,2017.Picha zote Kadama Malunde- Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kukataa kurubuniwa ili kuepuka mimba za utotoni.
Watoto wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro huku wakisoma vipeperushi vinavyohusu masuala ya watoto.
Mgeni rasmi Josephine Matiro (katikati ya watoto) akicheza muziki na wanafunzi,aliyevaa nguo nyekundu ni Afisa Utamaduni wa wilaya ya Shinyanga,Janeth Elias,aliyekuwa MC katika maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa kike.
Meneja wa Shirika la Kimataifa la Save the Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike kwa mkoa wa Shinyanga ambapo alisema mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni yanahitaji ushirikiano baina ya serikali,wazazi na mashirika na taasisi zinazohusika na masuala ya watoto.
Wanafunzi wakifurahia jambo wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya mtoto wa kike kimataifa.
No comments:
Post a Comment