Advertisements

Monday, October 16, 2017

MKUU WA MAJESHI: KIAMA CHA WASIOJULIKANA KIMEFIKA

Rais Magufuli akimwapisha Jenerali Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini. (Picha na Maktaba).

IKIWA ni zaidi ya mwezi tangu kujeruhiwa kwa kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliye pia Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Tundu Antipas Lissu na watu wanaoitwa ‘wasiojulikana’, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini, Jenerali Venance Mabeyo ameonya vikali juu ya matumizi ya silaha za kijeshi na kwamba kiama chao kimewadia.

Akijibu swali la mwandishi Sam Mahela kupitia Kipindi cha Dakika 45 cha ITV lililotaka ufafanuzi juu ya vitendo vya uhalifu na matumizi mabaya ya silaha za kijeshi, Jenerali Mabeyo alisema kuwa, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaaminika kimataifa na ndiyo maana limekuwa likiombwa kutoa misaada ya kiusalama katika nchi mbalimbali, hivyo haliwezi kushindwa kudhibiti matumizi mabaya ya silaha na matukio ya kihalifu na kuwataka wanaofanya vitendo hivyo waache mara moja vinginevyo kiama chao kimefika.

Aidha, kwa sauti nzito, yenye mamlaka na kujiamini, Jenerali Mabeyo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama katika kufichua watu wanaofanya

matendo ya kihalifu ili kusaidia ukomeshaji wa matukio hayo kwa watu wanaoitwa wasiojulikana ili kuitunza amani ambayo imekuwepo nchini.

“Kwanza tunawaomba sana wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vyetu vya usalama ili kupambana na hatimaye kukomesha matumizi haya mabaya ya silaha za kijeshi kutoka kwa wahalifu wasiojulikana ambao kimsingi hatutaki kuwasikia na kuwaona tena na hapa niseme tu ukweli kwamba mwisho wao umefika,” alisema Jenerali Mabeyo.

Kuhusu hali ya usalama kwenye mipaka yetu, Jenerali Mabeyo aliwatoa wasiwasi Watanzania kwa kusema kuwa, JWTZ kupitia vikosi vyake liko imara katika kulinda mipaka ya nchi kwani ndilo jukumu na kazi yake kubwa hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na badala yake wajikite zaidi kufanya kazi kwa nguvu ili kujiletea maendeleo binafsi na uchumi wa taifa kwa jumla.

Kuhusu baadhi ya watu wanaolichafua Jeshi la Wananchi kwa kujifanya askari na kutapeli kwa lengo la kujipatia kipato ikiwa ni pamoja na kuwadanganya watu watoe fedha kwa ajili ya kuwafanyia mipango ya ama wao au vijana wao kujiunga na jeshi hilo, alisema kuwa tayari wameshakamatwa vijana kadhaa na oparesheni bado inaendelea huku akitahadharisha watu waache kufanya hivyo kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Juu ya namna ambavyo Jeshi la Wananchi linakabiliana na mabadiliko ya ulimwengu wa teknolojia, Jenerali Mabeyo aliiomba serikali kusaidia kwa ajili ya vifaa vya kisasa ili kukabiliana na mabadiliko hayo na kwamba wanaajiri pia vijana wenye ujuzi na sifa mbalimbali zinazohusiana na mabadiliko hayo.

Jenerali Mabeyo alifafanua namna ambavyo askari wa Jeshi la Wananchi wamekuwa wakinufaika wanapokwenda kulinda usalama wa nchi mbalimbali kupitia Jeshi la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo alisema:

“Upo utaratibu, ambapo Umoja wa Mataifa huiomba nchi kisha kuiuliza nchi husika kama wanakubali Tanzania ikalinde amani na kama wakikubali, basi tuna makubaliano maalum. Kwa mfano kama askari akipata ulemavu au kifo, namna ambavyo yeye au familia yake itanufaika, kwa kweli ni mambo mazuri lakini pia wanapata kipato cha ziada, ukiondoa malipo yao ya kawaida kama mshahara ipo posho ya ziada ambayo wanalipwa na kwa kweli imekuwa ikiwasaidia sana kwa uchumi.”

 STORI: BRIGHTON MASALU | IJUMAA WIKIENDA | DAR

No comments: