Mushi alifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akisoma mashitaka hayo, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Vitalis Peter alidai kati ya Machi 21, mwaka jana na Juni 30, mwaka jana katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa TRA, mshitakiwa huyo alikutwa akimiliki magari 19 ambayo ni mali zisizolingana na kipato chake.
Alitaja magari hayo kuwa ni Toyota Rav 4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark ll, Toyota Regiusage, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Lasso, Suzuki Carry, yote yakiwa na thamani ya Sh 197, 601,207.
Katika mashitaka ya pili, inadaiwa kuwa kati ya Machi 21,2012 na Machi 30, mwaka jana, Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA aliishi maisha ya kipato cha juu tofauti ya thamani ya Sh 333, 255,556, tofauti na kipato chake.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo, umekamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa maelezo ya awali.
Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Elisalia Mosha aliomba mahakama hiyo kumpatia dhamana mteja wake kwa sababu mashitaka aliyonayo yanadhaminika kisheria. Hakimu Shaidi alimtaka mshitakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja, atakayesaini bondi ya milioni 20 na mshitakiwa alikidhi masharti ya dhamana.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment