Katika makubaliano hayo yaliyomleta nchini Mwenyekiti wa Barrick Gold, Profesa John Thornton kwa ndege binafsi kutoka Canada mara mbili, Tanzania imepata kile ambacho nchi chache duniani zilifanikisha katika majadiliano yaliyozinufaisha sekta ya madini Kama sehemu ya makubaliano, Kampuni ya Barrick imekubali kulipa Dola za Marekani milioni 300 (zaidi ya Sh bilioni 700) kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo, huku mazungumzo zaidi yakiendelea, hatua ambayo Rais Magufuli ameiita kuwa ni mwanzo mzuri wa kudhibiti maliasili zetu na mapato yatakanayo nazo.
Pamoja na kupewa hisa asilimia 16 katika migodi yote ya Barrick nchini, makubaliano hayo pia yanaruhusu Tanzania kuchukua madini yanayopatikana baada ya makinikia kuuzwa huku ikipata mgawo wa faida ya nusu kwa nusu na Barrick pale dhahabu ya kawaida inapouzwa.
Aidha, Barrick itaweka ofisi zake mpya katika jiji la Mwanza Tanzania na idadi ya Watanzania wanaoshiriki katika Bodi na menejimenti ya kampuni itaongezeka ili kulinda maslahi yake. Ndiyo maana katika makala yake yaliyoitwa “Tanzania’s squeeze on mining firms seems to be working as it gets $300 million in back taxes” Jarida mashuhuri la masuala ya madini Quartz lilimweleza Rais Magufuli kama kiongozi aliyefanikiwa kuzibana kampuni kubwa kwa maslahi ya wananchi wake na hayumbishwi.
“Rais wa Tanzania mwenye msimamo usioyumba katika madini, Dk John Magufuli anaongoza vita inayohakikisha kuwa kampuni kubwa zinapata haki yao lakini wananchi wa Tanzania nao wanapata faida katika sekta ya madini,” anaandika Abdi Latif Dadir mwandishi wa jarida hilo la Marekani.
Mtandao wa habari za uchumi na biashara wa Bloomberg ulisema Rais Magufuli ni kiongozi “anayeifanyia mageuzi makubwa sekta ya madini ili iwafaidishe wananchi wa Tanzania.” Mtandao huo pia umeongeza kuwa licha ya azma hiyo, Serikali ya Magufuli pia ina mikakati mipana zaidi “kutekeleza sera ya viwanda na miradi ya kiuchumi katika nchi ambayo ni ya sita kuwa na uchumi mkubwa katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Sahara.”
Gazeti mashuhuri la New York Times lilisema Serikali nyingi Afrika na Asia-kutoka Afrika Kusini hadi Indonesia zimeanzisha harakati za kuhakikisha zinafaidika zaidi na maliasili zao. Gazeti hilo limeeleza hatua alizozichua Rais Magufuli ikiwemo kuzuia usafirishaji wa mchanga wa madini maarufu kama makinikia.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment