ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 8, 2017

MWENYEKITI MPYA CCM (W) YA MANYONI ACHAGULIWA ATEMA CHECHE ATAKA KUIONA MIKATABA YA MALI ZOTE ZA CHAMA

Mwenyekiti mpya wa CCM Wilaya ya Manyoni aliyechaguliwa kwa kura za kishindo na wajumbe wa mkutano Mkuu wa CCM Wilaya Ndg Jumanne Ismail Makhanda akiwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua katika nafasi hiyo.
 Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi wakishangilia mara baada ya kutangazwa matokeo ya kura walizopiga.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza jambo wakati wa Mkutano maalumu wa CCM Wilaya ya Manyoni.
Zoezi la upigaji kura katika Mkutano maalumu wa CCM Wilaya ya Manyoni.
Zoezi la upigaji kura katika Mkutano maalumu wa CCM Wilaya ya Manyoni.
Zoezi la upigaji kura katika Mkutano maalumu wa CCM Wilaya ya Manyoni.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa CCM katika wilaya ya Manyoni Katibu wa siasa na uenezi wa Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mhe Mussa Sima akizungumza jambo wakati wa Mkutano Mkuu maalumu wa CCM ngazi ya Wilaya.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu maalumu wa CCM Wilaya ya Manyoni wakifatilia kwa makini mkutano uliiokuwa na agenda ya upigaji kura.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu (Katikati) Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa CCM katika wilaya ya Manyoni Katibu wa siasa na uenezi wa Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mhe Mussa Sima (Kushoto) na Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Hemed Fereji wakifurahi jambo mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi.


Na Mathias canal, Singida


Wajumbe wa Mkutano mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kwa kauli moja wametumia haki yao ya kidemokrasia kwa kufanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa ngazi mbalimbali za Wilaya, wawakilishi wa ngazi ya mkoa na Taifa.


Mkutano huo ulifanyika katika Viwanja vya CCM eneo la Mjini kati, Kata ya Manyoni Mjini na kuhudhuruwa na wajumbe waliozidi akidi ya matakwa ya mkutano wa CCM Wilaya kwa mujibu wa maelekezo ya kanuni za uchaguzi wa CCM.


Mwenyekiti mpya wa CCM Wilaya ya Manyoni aliyechaguliwa kwa kura za kishindo ni Ndg Jumanne Ismail Makhanda kwa kupata 842, nafasi ya pili imeshikiliwa na Elia Abrahamu kwa kupata kura 199 na Geofrey Caratta aliyeshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 29.


Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi katika nafasi hiyo Mwenyekiti Jumanne Makhandi amemtaka katibu wa Chama hicho Wilaya ya Manyoni kuandaa taarifa na mikataba ya mali zote za chama ikiwemo nyumba na fremu za Maduka namna ya uwekekezaji ulivyo ili kubaini ubadhilifu wa mali za chama.


Alisema kuwa ni jambo la aibu kwa viongozi mbalimbali wa CCM hususani watendaji wa mashina, Matawi na Kata kutumia gharama zao kueneza na kufanya shughuli za chama ilihali kuna mali nyingi za chama zisizo eleweka namna zinavyotumika.


Aliahidi kutekeleza na kusimamia ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 huku akiwashi wananchi kwa kauli moja kushirikiana na Viongozi wote wa Chama na serikali hususani kumuunga mkono Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia wananchi pasina kujali maslahi yake binafsi. 


Aidha, Alisema kuwa wananchama wanapaswa kuzifahamu mali zao zitokanazo na nguvu zao katika chama ikiwa ni pamoja na kusomewa mapato na matumizi ili kuondoa ombwe la malalamiko na sintofahamu baina ya wananchama na uongozi wa chama.


Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu aliwasihi wajumbe wote kuwaunga mkono washindi wa nafasi zote za uongozi ndani ya CCM ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika kuwatumikia.


Mhe Mtaturu alisema kuwa katika kipindi cha uchaguzi wa ngazi ya chama na hata serikali kila mwananchi huwa na maono na mtazamo wake kwa kiongozi amtakaye lakini pindi anapochaguliwa kiongozi mmoja ni wazi ni vyema ikawa mwisho wa makundi hayo hivyo kuwa na mshikamano mpya katika uwajibikaji.


Naye Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo wa CCM katika wilaya ya Manyoni Katibu wa siasa na uenezi wa Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mhe Mussa Sima aliwapongeza wananchama kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura, jambo alilosema wametumia vyema haki yao ya msingi ya kupiga kura kwa mujibu wa katiba ya CCM.


Pia alimpongeza Mwenyekiti mpya wa CCM kwa kuanza kutema cheche za uwajibikaji katika nafasi yake huku akisema kuwa ni viongozi wachache wenye uwezo kama wake wa kuthubutu.


Nafasi zingine zilizowaniwa ni Ujumbe wa Mkutano Mkuu CCM Mkoa ambapo waliopata uwakilishi huo ni Leah Gervas Haule aliyepata kura 570 na Abasi Jumanne Mayeye aliyepata kura 490. 

Wengine ni wajumbe wa mkutano mkuu CCM Taifa ambao ni Eliza Bajile kura 480, John Lwanji aliyepata kura 417 na Neema Ukota aliyepata kura 399.


Wengine ni wajumbe wa wa Halmashauri Kuu CCM Wilaya ambao ni Widon Mathayo aliyepata kura 610, Zabibu Shaibu kura 470, Jofrey Farijala kura 394, Hussein Masawo 390, Lucy Mtinya 381, Abeli Razalo 361, Sauda Masabuni 327, Wahida Magili 311, Juma Mwendi 301 na Shakira Hema aliyepata kura 289.

Nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Manyoni imenyakuliwa na Said A. Mohamed aliyemshinda mshindani wake kwa tofauti ya kura 12 ambaye ni Gervas Simion aliyepata kura 70.


MWISHO

No comments: