Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiwa katika moja ya ziara zake alizozifanya hivi karibuni Mjini Zanzibar
Na. Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali imejenga kuta na kupanda mikoko katika fukwe mbalimbali hapa nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yalikuwa yakisababisha uhalibifu mkubwa katika fukwe hizo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Januari Makamba wakati wa mahojiano katika kipindi cha "TUNATEKELEZA" kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1) kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu Tano.
“Tumeamua kutafuta fedha ili kupanda mikoko na kujenga kuta ili kudhibiti fukwe kuliwa na bahari,” alisema Makamba.
Aidha, amesema kuwa, mabadiliko ya tabia ya nchi katika fukwe za bahari yamesababisha kupotea kwa maeneo ya kilimo kutokana na maji ya bahari kuingia katika mashamba na kuharibu mashamba hayo ambayo mengi ni ya mpunga.
Makamba amesema kuwa ujenzi wa kuta na upandaji wa mikoko utasaidia kulinda mashamba hayo kutoingiliwa na maji ya bahari pamoja na kuzilinda fukwe za bahari ambazo ni moja ya vivutio vya utalii wa nchini.
“Bila kuhifadhi mazingira hakuna utalii, uzuri na ubora wa fukwe unategemea fukwe hizo kutoliwa na maji ya bahari” alifafanua Makamba.
Kwa upande wa Muungano, Makamba amesema Wizara yake imefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa bara na visiwani likiwemo suala la usafirishaji wa magari kwa pande zote mbili.
“Kulikuwa na malalamiko mengi juu ya kutotambulika kwa magari yanayotoka upande wa Bara kutotambulika upande wa Visiwani, hivyo hivyo kwa magari yanayosajiliwa upande wa Visiwani kutotambulika upande wa Bara. Tumelisimamia na kutaka kulimaliza katika sheria mpya za usalama barabarani” alifafanua Makamba.
Makamba amesema, makubaliano ya sheria hiyo mpya yameshafanyika na kamati za pamoja zaTanzania Bara na Visiwani zimepitisha sheria hiyo.
No comments:
Post a Comment