Wanafunzi wa Shule za Msingi
zilizopo Kata ya Kiwalani wakishiriki igizo lenye lengo la kuelimisha
jamii umuhimu wa kunawa mikono na majisafi na sabuni wakati wa kilele
cha wiki ya unawaji mikono kwa maji na sabuni yaliyofanyika kata ya Kiwalani jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka wananchi kuunga mkono juhudi za usafi kwa kunawa
mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu ili
kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora.
Akizungumza katika kilele cha wiki ya unawaji mikono kwa maji na sabuni
iliyofanyika Kata ya Kiwalani, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Ubora wa Mamlaka ya Majisafi na
Majitaka Dar es Salaam(DAWASA), Dk Sufiani Masasi alisema kama Taifa ni
muhimu kuwekeza nguvu katika kuelimisha jamii hasa umuhimu wa kunawa
mikono na majisafi na sabuni ili kujenga Taifa lenye afya bora.
Akizungumza na jumuiya ya wananchi, waalimu na wanafunzi wa shule za
msingi Umoja, Yombo, Mwale na Bwawani, Dk Masasi alisema DAWASA ni mdau
muhimu wa usafi wa mazingira ndio sababu waliamua kuadhimisha wiki hiyo
kwa kutoa elimu kwa walimu 44 kutoka katika shule hizo pamoja na baadhi
ya viongozi wa serikali ya mtaa ili wawe mabalozi
Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Mikono safi kwa
manufaa ya sasa na baadae’ inaikumbusha jamii kuona umuhimu wa kunawa
mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu.
Hivyo alitaka juhudi za pamoja zichukuliwe kuhakikisha wanafunzi
wanaelewa umuhimu wa kunawa mikono kwani wao ndio wazazi wa siku zijazo
na kwamba DAWASA itaendelea kuunga mkono kampeni za usafi hasa kwa
kuendelea kubuni na kutengeneza miundombinu ya majisafi katika Maeneo
mbalimbali ya jiji.
Dk Masasi alisema tayari DAWASA imefanikiwa kufikisha mradi huo wa
majisafi kwa shule hizo ambapo utanufaisha wanafunzi 5123 pamoja na
zahanati ya eneo hilo na kwamba itaendelea kufadhili miradi ya aina hii
ili kuunga mkono juhudi hizo za usafi wa mazingira.
Mkufunzi wa mafunzo kwa walimu wa shule hizo, Juhudi Nyambuka ambaye ni
Afisa Afya Manispaa ya Temeke alipongeza juhudi za DAWASA katika
kusaidia jamii kupata huduma za majisafi na kueleza zitasaidia kupunguza
magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji.
Katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma rasmi za maji ya bomba
DAWASA, jumuiya za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo wamekuwa
wakijenga miradi ya maji kupitia programu ya maji na usafi wa mazingira
kwa jamii.
Miradi hiyo ipo katika maeneo mbalimbali kama vile Ukonga, Yombo, Kitunda, Mbagala, Kijichi, Feri,Kigamboni
Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha
No comments:
Post a Comment