Advertisements

Saturday, October 21, 2017

SHAHIDI AIELEZA MAHAKAMA JINSI SCORPION ALIVYOMTOBOA MTU MACHO

Mahakama ya Wilaya ya Ilala Oktoba 31, 2017 itatoa uamuzi iwapo mshtakiwa Salum Njwete maarufu Scorpion ana kesi ya kujibu au la.

Uamuzi utatolewa baada ya jana  Ijumaa Oktoba 20,2017 upande wa Jamhuri kufunga ushahidi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi ikiwemo kumtoboa macho, Said Mrisho inayomkabili Njwete (34).

Katika hati ya mashtaka, Njwete anayewakilishwa na wakili Juma Nassoro anadaiwa kutenda makosa hayo Septemba 6,2016 saa nne usiku eneo la Buguruni wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka, Salum Masoud mkazi wa Buguruni ambaye ni mfanyabiashara wa kuuza chenji katika kituo cha daladala amedai siku ya tukio alikuwa katika biashara zake.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule alidai akiwa katika shughuli zake alishuhudia mabishano kati ya mshtakiwa na mteja aliyekuwa akinunua bidhaa eneo hilo.


Amedai alimuona mshtakiwa akigonga meza akimlazimisha mteja huyo kumfuata. Shahidi huyo alidai mteja huyo alishangaa kuitwa na mtu asiyemfahamu hivyo alikataa kwenda.

Masoud alidai alimuona mshtakiwa akimfuata mteja huyo, kumvuta, kumwangusha chini na kuanza kumpiga maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Amedai alimwona mshtakiwa akichomoa kisu na kumtoboa mteja huyo na alisikia sauti ya kilio chake cha kuomba msaada, huku akitokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Shahidi huyo alidai mshtakiwa alichukua mkufu aliokuwa amevaa mteja huyo shingoni na uliokuwa mkononi. Pia, alidai alichukua pochi iliyokuwa mfukoni na alimsukuma kwenye Barabara ya Mandela ambako alianguka.

Baada ya mshtakiwa kuondoka, Masoud anadai walimnyanyua mteja huyo na kumweka eneo la wazi linalotenganisha barabara.

Amedai mtu aliyekuwa eneo hilo alitoa taarifa polisi ambao walifika eneo hilo na kuwatawanya kabla ya kumchukua majeruhi na kumpeleka hospitali.

No comments: