Advertisements

Wednesday, November 22, 2017

Kafulila ajivua uanachama wa CHADEMA

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye Desemba mwaka jana alijiunga na Chadema, ametangaza kung’oka upinzani kwa madai hauna dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi.
Kafulila aliyekuwa mbunge 2010-2015 alitikisa kwenye mapambano ya sakata la ufisadi wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow iliyoitikisa serikali katika utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ametangaza uamuzi huo leo Novemba 22.
Akizungumza na Mwananchi kuthibitisha waraka wake alioutoa wa kujivua uanachama wa Chadema amesema ‘’ni kweli nimeondoka na siwezi kusema nakwenda wapi kwa sasa.”
Katika waraka huo, Kafulila amesema tangu Rais John Magufuli achaguliwe na kukabidhiwa jukumu la kuongoza nchi, vita ya miaka mingi dhidi ya ufisadi imechukua sura mpya.
“Wahusika na watuhumiwa wakubwa wa rushwa ambao walikuwa hawaguswi huko nyuma tunashuhudia wakifikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Kutokana na juhudi za kupambana na rushwa na ufisadi zinazoendelea nchini…juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono,” amesema Kafulila
“Vyama vya upinzani vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika juhudi zake za kupambana na ufisadi. Ghafla ufisadi sio tena agenda kuu ya vyama vya upinzani nchini, kwa sababu hii, ni wazi kuwa upinzani sio tena jukwaa salama la kuendesha vita dhidi ya ufisadi,” ameongeza
Kafulila ambaye ni mme wa mbunge wa viti maalum Chadema, Jesca Kishoa amesema ‘’kwa kuwa sina imani tena na upinzani kama jukwaa salama la kupambana na ufisadi, nimeamua kwa hiari na utashi wangu kujivua uanachama wa Chadema kuanzia leo.”
“Nitatangaza katika siku za hivi karibuni jukwaa jipya la harakati zangu dhidi ya ufisadi. Nawatakia safari njema waliobaki ndani ya Chadema kwa kile wanachokiamini.”

Chanzo: Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Ameahidiwa cheo kama ambavyo Dr. Slaa alivyofanya. Atapewa ukuu wa wilaya hakuna jingine. Hivyo wewe Kafulila huoni aibu kusema kuwa ufisadi umeondoka kuwa agenda kwenye upinzani? Kwani wewe kwa akili yako kwa miaka 50 iliyopita upinzani walihusika na ufisadi? TANU/CCM ndiyo walioharibu nchi yetu na ufisadi kutamalaki. Kwanini unakuwa muongo hivyo???? Unakwenda kwenye jukwaa la CCM kwa ajili ya cheo wala si kingine ila usaliti utalipwa hapa hapa duniani. Dr Slaa leo atafurahi kuona ameshinda lakini angejua anachokipata ni kidogo kuliko kile ambacho angekipata pamoja na heshima....ATAFURAHIA UBALOZI? Kweli watanzania bado tupo mbali mno, wanapiga kelele lakini wakipewa ubalozi, ukatibu, ukuu wa mikoa/wilaya, na vyeo vidogo wanasahau malengo yao.

Anonymous said...

Anonymous wa 3:41 PM una fikra finyu. Unadhani kuwa mwanaChadema ndiyo kuleta mabadiliko au maendeleo? Miaka mingapi imepita na wapi Chadema ipo? Ukabila na ukanda ndicho kinachowaua.