Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema ataripoti polisi mkoani Morogoro kuitikia wito wa jeshi hilo.
Heche amesema ataripoti polisi Jumatatu Novemba 20,2017 kwa kuwa ana taarifa kwamba anatafutwa na jeshi hilo.
Polisi walioelezwa kutoka mkoani Morogoro jana Ijumaa Novemba 17,2017 walifika eneo la Bunge na Heche alilieleza Mwananchi kuwa walimpatia wito kuwa anatakiwa kwenda kuhojiwa mkoani Morogoro.
Heche pia alieleza hofu yake kwamba polisi walikuwa wamkamate, hata hivyo hilo halikufanyika.
Mbunge huyo alisema hajui kosa alilotenda, isipokuwa anatakiwa kuhojiwa kwa kauli alizotoa alipomsindikiza mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali alipotoka gerezani.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Novemba 18,2017 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema mbunge huyo alifanya mkutano wa hadhara wilayani Kilombero Aprili 8, 2017.
Kamanda Matei alisema wanamtafuta Heche kwa kosa la kutotii amri za viongozi na kufanya mkutano Kilombero na kutoa lugha ya matusi hivyo kutaka kusababisha vurugu.
Polisi iliandika barua kwa Spika wa Bunge kumtaarifu kuwa mbunge huyo anatafutwa kwenda kujibu tuhuma zinazomkabili mkoani Morogoro.
"Barua ni mambo ya siri kati ya jeshi na Bunge, tunachotaka sisi ni kumuona Heche hapa na asitake tutumie nguvu," amesema Kamanda Matei alipoulizwa kuhusu barua waliyoiandika kwa spika.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment