Advertisements

Thursday, December 28, 2017

MAUAJI, UTEKAJI NYARA NA UTESAJI SIYO UTAMADUNI WETU

Nashawishika kuandika Makala haya kuyasema yaliyotokea, yanayotokea na yale nayoyaona kama yanaendelea kutokea sasa hivi. Kama mtanzania na alivyo mtanzania yoyote yule ninayo haki ya msingi kutoa mawazo yangu na kukemea yale nayoyaona hayafai bila kutishwa na yeyote yule…Hii ni nchi yetu sote siyo nchi ya Umoja wa vijana wa CCM, jumuiya ya wazazi au UWT (CCM). Katiba inasema binadamu wote ni sawa, kila mwananchi ana haki ya kuishi bila bugudha na kutoa maoni yake na kusikilizwa na bila kuonewa (Reprisal),kuna kipengele kinachosema cheo ni dhamana yaani hivi vyeo walivyonavyo hao viongozi wetu si vya milele na haviwafanyi kuwa wao bora zaidi kuliko wengine bali ni dhamana watakayowaachia wengine muda wao utakapoisha ( Non-dynasty).

Kumekuwa na vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa na serikali hii ya John Pombe Magufuli kila mmoja anaviona lakini kwa vile wengi wetu tumejengwa uoga tunashindwa kusema na kukemea, Kama kuna siku wakifufuka akina Mkwawa, Mirambo, Meli, Sina, Kinjekitile, Abushiri na mashujaa wengine waliopigana na kusimama imara dhidi ya wakoloni hakika watatucheka na kushangaa kuona wakoloni weusi waliojipangia daraja la juu wakiwanyanyasa vya kutosha na kuwaua kwa kutoa mawazo yao tu, kweli watasikitika sana!

Bado hatujasahau na hatutasahau upigwaji wa risasi nyingi ( Assassination attempt ) kwa Tundu Lissu, utekwaji na upoteaji wa mamia ya watanzania akiwemo Ben Saanane (Zaidi ya mwaka sasa), Azzory Gwanda ( leo siku ya 31, Mkubwa wa polisi anajua alipo lakini anajibu kwa kejeli kuwa “Atarudi tu” jibu jepesi na la dharau) na wengine huko Kibiti na sehemu mbalimbali za nchi yetu bila maelezo ya kuridhisha, upatikanaji wa maiti zenye dalili za kuteswa katika fukwe zetu za bahari na mito….. hakuna anayeweza kubisha kuwa si kazi ya vyombo vya dola hasa polisi na hayo magari meupe yanayofuatilia watu wasio na makosa kwa sababu tu wametoa maoni yasiyoendana na mawazo yao au yasiyowasifu……..ambayo kikatiba ni haki ya msingi kwa kila mtanzania! Serikali hii inataka uwasifu tu hata kama hakuna ukweli kwenye wanalofanya.

Tundu Lissu alitoa ushahidi wa kukamatwa kwa Bombardier iliyonunuliwa na serikali kule Canada ingawa serikali ilificha kwa sababu inazozijua yenyewe, tunachokijua ni hasira kali ya serikali (rage) dhidi yake. Ben Saanane alipotea baada ya kuhoji Shahada ya Uzamivu ya rais akaviziwa na kutekwa, Roma Mkatoliki kama msanii aliimba jambo aliloliona kama kero kwake…akakamatwa na kupewa mateso asiyo stahili, Nay wa Mitego alikamatwa kwa kuimba wimbo wanaohisi ulimtaja rais… alikamatwa na kulala mahabusu Zaidi ya saa 48 kinyume cha sheria, Orodha ni ndefu ya walioteswa na kulala mahabusu! Kila mmoja wetu ni shahidi.

Rais ni taasisi na wala siyo mtu binafsi, upinzani wa kistaarabu dhidi ya rais haukwepeki!. Donald Trump na “Birthers” wenzake walikuja na conspiracy theory juu ya mahali alipozaliwa Obama……Mbona hakukamatwa? Hii Demokrasia yetu ina matatizo gani? Ninachoweza kusema hii demokrasia yetu inawapendelea hao mnaowaita viongozi na familia zao na kuwakandamiza wananchi wa kawaida. Leo ukiongea jambo ambalo serikali halipendi kusikia kama katiba mpya,uonevu wa polisi dhidi ya wapinzani n.k utaanza kuhangaishwa kwanza kuhusu uraia wako, utasingiziwa unatoka Rwanda, Burundi, Uganda au nchi nyingine yoyote jirani….

Askofu Niwemugizi aliongea kuhusu katiba mpya akahojiwa na uhamiaji, Askofu Niwemugizi alizaliwa kabla ya Uhuru wa Tanganyika sawa na Magufuli na ushahidi wa kuzaliwa Tanganyika haupingiki lakini Magufuli na genge lake wanajaribu kuwaaminisha watu kuwa Askofu huyo ambaye tangu amezaliwa hakuulizwa uraia wake kuwa uraia wake una mashaka! Aibu. Tarehe 12/13/17 zimeokotwa maiti nyingine 4 zikiwa zimefungwa kwenye viroba na kufungwa mawe mazito….staili ile ile kwa maiti 17 zilizookotwa kwenye fukwe hizo hizo kwa muda wa miezi mitano mfululizo iliyopita. Mpaka lini watauawa watu wasio na hatia na miili yao isizikwe bali kufungwa kwenye viroba?

Magufuli siyo mcha Mungu kama anavyojinasibu mwenyewe ni chui aliyejificha kwenye ngozi ya kondoo, anafahamu na anabariki yote yanayoendelea kuanzia uvamizi wa Clouds TV/Radio, utekaji nyara wa Roma Mkatoliki, kupotea kwa Ben Saanane, kulipuliwa kwa bomu kwa ofisi za mawakili, kupigwa risasi katika jaribio la kumuua Tundu Lissu na UCHAFU WOTE MWINGINE ALIOFANYA NA ANAOENDELEA KUUFANYA.

Watanzania tumejaa uoga hata tukionewa tunakwenda kikondoo kondoo, wengi wetu watasema wanamwachia Mungu hatusimami katika misimamo imara ndiyo maana tunaendelea kudharaulika na Wakenya kwa sababu ya uoga wa kushindwa kudai haki zetu za msingi! Baada ya kutekwa Roma Mkatoliki ameshindwa kujieleza na kuyaeleza yaliyompata anaongea kimafumbo fumbo……TUTAENDELEA KUTEKWA kwa sababu watekaji wanajiona wana nguvu na hakuna wa kuwafanya lolote, watekwaji wapo kimya……KIMYA! KIMYA! KIMYA! Dr. Ulimboka alinyamaza kimya pamoja na mateso yote ya kung’olewa meno na vipigo vya nguvu…..

Tusubiri kusikia amehamia CCM kwa kufurahishwa na kazi nzuri mwenyekiti Magufuli anayofanya! Rais Benjamin Mkapa alisema “WATANZANIA NI WAVIVU WA KUFIKIRI” hakukosea! Haitoshi watalii kuja kutazama Wanyama tu nchini kwetu bali waje kutushangaa Watanzania kwa sababu ya tabia zetu za ajabu ajabu, Utamaduni wetu ni wa kuchekesha na kusikitisha……..

siyo rahisi kuamini tunapewa Khanga na Pilau ili tukichague chama tawala CCM, baada ya uchaguzi kwisha Pilau, Khanga, T-shirts na Kofia zinakoma tunarudi kwenye umaskini wa kutupwa uliosababishwa na chama hiki hiki. “We must be good candidates for culture tourisms than our East Africa’s peers” Hilo halina ubishi….Kama kuna sehemu watu wamekaa vijiweni wanasubiri mtu afe ile wakale Pilau katika karne hii ya 21 basi kuna tatizo tena kubwa mno! Labda tutahitaji Maombi ya Pope, Mufti, Dalai Lama, Kadhi, Maaskofu,Masheikh na viongozi wa dini za jadi ili hizi tabia hizi zibadilike, Hao viongozi wanatumia mbinu mbalimbali kuwanyima elimu tuendelee kuwa maskini wa akili ili waendelee kututawala.

Rais Magufuli ana bahati ya kuokota vitu….Alikwenda Bandari ya Dar eS Salaam mara ya kwanza kaokota vichwa vya Treni 13 ambavyo havina mwenyewe na haijulikani jinsi vilivyofika hapo Bandarini…HAKUNA MWENYE NAVYO, sarakasi ikaanza Profesa Mbarawa akasema watavinunua wakiona ni vizuri….Watanunua kutoka kwa nani?? Tanzania nani anamiliki Treni? Mara ya pili akaenda Bandarini akaokota tena gari za kubebea wagonjwa (ambulances)58 ambazo hazina mwenyewe, serikali wakiona itapendeza watanunua kutoka kwa asiyejulikana! Hizo TRANSACTIONS zitafanyikaje wakati muuzaji hajulikani hadi leo?

Tukio la uchaguzi wa madiwani hasa wa wilaya ya Arumeru tuliona jinsi wawakilishi wa vyama vya upinzani walivyotolewa nje baada ya kugundua maboksi ya kura yakiwa yamejazwa karatasi za kura asubuhi kabla hajaingia mpiga kura hata mmoja, rais anaelewa na kila mmoja wetu anajua hilo lakini bila haya huyo rais anafungua mdomo wake kujitapa kuwa wameshinda ushindi wa kishindo ( Landslide winning)…Hivi kweli sehemu ambayo hamuwezi kushinda mnaweza kushinda kwa kishindo? Ndiyo maana nasema huyo Rais siyo mcha Mungu kama anavyojinasibu! Sishangai ndiyo maana hata alikimbilia kwa babu wa Loliondo kunywa Kikombe cha maji ya uchafu….Aibu aibu aibu !!

Maaskofu wamezungumza Katiba, Uonevu wa Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi wa kawaida na wa upinzani, Upoteaji, Utesaji, Utekwaji, Mashambulizi ya risasi na mapanga na Mauaji ya wananchi wasio na hatia. Tumeona kundi la wanaojiita makada wa CCM wakitishia kuwachukulia hatua kwa kuwataka vyombo vya usalama kuwashughulikia!! UTADHANI NCHI HII INAMILIKIWA NA CCM! Lini huo ulevi utawaisha? WAMEJISAHAU WANAAMRISHA POLISI kama vile ni moja ya jumuiya ya CCM! Nchi hii ni yetu sote siyo ya CCM…..Inaweza kushinda chama chochote au mgombea binafsi lakini wakiongoza tumewapa dhamana.

Rais Magufuli anasema amesukumizwa tu kushika madaraka! Siku nyingine akisahau anasema hajawekwa na mtu, ni kweli amesukumiziwa…….Kumbukumbu zinaonyesha mwenyekiti wa CCM Kikwete aliingia na majina yake mfukoni akimtaka mtu wake, yeye Magufuli aliyewekwa kama msindikizaji akasukumizwa baada ya mchezo kugeuka! Sasa Magufuli atasemwa alifika hapo alipo Mwenyewe? Kikwete juzi kwenye mkutano wa CC wa CCM alisema alipata kazi sana kumuuza kwenye Kamati kuu kwa sababu hakuwa na ”experience” hata ya uwenyekiti wa mtaa sembuse atawezaje kuwa mwenyekiti wa CCM? Mpaka hapo atasema hajabebwa? C’mon Magufuli acha kujificha wakati tunakuona. Ungepaswa pia umshukuru sana Lowassa aliyebadilisha upepo wa yeye na wajumbe waliomtaka, kumkataa Benard Membe na wewe kubaki ”only alternative” Bado unaendelea kubisha? Ungetakiwa umheshimu sana Edward Lowassa!

Magufuli utafunga watu wangapi au utawapoteza watu wangapi kwa kukupinga? Ben Saanane amepotea, Azory Gwanda leo ni zaidi ya Mwezi mmoja amepotea lakini waliomchukua wanafahamika….Nissan nyeupe iliyomchukua ni kama ile iliyotumika katika kumshambulia Tundu Lissu (Namba mlishatajiwa lakini mmekaa kimya kwa sababu mnajua mliwatuma kina nani) Damu ya watu haitapotea bure, Hao mnaowafunga kwenye viroba baada ya kuwatesa na kuwaua bila kuwafikisha kwenye mikondo ya sheria kama wamekosa damu yao haitapotea bure….Ipo siku mtaulizwa tu, IT IS A DISGRACE TO HAVE MAGUFULI AS A PRESIDENT! Hafai tunajua historia ya alipotoka maisha hayana thamani ndiyo maana wazee na vikongwe wanaendelea kuuawa, wenye ulemavu wa ngozi wanauawa kwa ushirikina…….Inaweza ukawa ni utamaduni wenu lakini hilo halipaswi kutokea kwenye nchi yetu, Watanzania wengi ni wastaarabu na wacha Mungu.

No comments: