AMINI usiamini, Simba inakaribia kuwa timu ya pili ghali zaidi Afrika mara tu itakapomaliza kuusajili mchakato wa mabadiliko kwenda kwenye mfumo wa hisa uliopitishwa klabuni hapo na kupata baraka zote za Serikali.
Bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ tayari ameshinda zabuni ya kuwa mwekezaji mkubwa ndani ya Simba akipewa asilimia 49 ya hisa za klabu hiyo kwa Sh20 bilioni na sasa kinachosubiriwa ni kukamilisha tu taratibu za kiofisi kuifanya Simba kuwa timu inayomilikiwa na Wanahisa.
Wanachama wa Simba watabaki na asilimia 51 licha ya kwamba awali walikubali kuimiliki timu hiyo kwa asilimia 50 na nyingine zimilikiwe na MO, lakini Serikali ikagoma.
Kwa mantiki hiyo jumla ya hisa zote za Simba zitakuwa na thamani ya Sh42 bilioni hivyo kuwa klabu ya pili ghali zaidi Afrika, ikiiacha mbali Yanga ambayo ndiyo kwanza imeanza mchakato wa mabadiliko.
Kwa mujibu wa mtandao wa Garbersports.com, kwa sasa klabu ghali zaidi Afrika ni Al Ahly ya Mirsi ambayo thamani yake ni Sh50 bilioni (Euro 19.25 milioni).
Klabu ya pili itakuwa Simba ikiwa na thamani ya Euro 15.9 milioni huku ya tatu ikiwa Esperance ya Tunisia ambayo thamani yake kwa sasa ni Euro 12.17 milioni (Sh33.6 bilioni)
Tunisia inaonekana kulishika zaidi soka la Afrika kwani Club Africain kutoka nchini humo inashika nafasi ya nne ikiwa na thamani ya Sh31.1 bilioni (Euro 11.8 milioni).
Tano Bora inafungwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo ina thamani ya Euro 10.48 milioni (Sh 27.6 bilioni).
Kwa upande wa Afrika Mashariki na Kati, klabu ghali zaidi ilikuwa TP Mazembe ambayo ina thamani ya Sh20.3 bilioni, ambazo ni sawa na fedha alizotoa MO kununua asilimia 49 tu ndani ya Simba.
Deni la mafanikio
Simba sasa itakuwa na deni kubwa la kuanza kufukuza mafanikio ya Al Ahly ambayo ndiyo klabu ghali zaidi Afrika.
Al Ahly ndiyo timu iliyoshinda mataji mengi zaidi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifanya hivyo mara nane, jambo ambalo linathibitisha kuwa inastahili kuwa namba moja Afrika.
Al Ahly imeshinda pia taji moja la Kombe la Shirikisho.
Mafanikio makubwa zaidi ya Simba katika michuano ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi (robo fainali) ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 na fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.
TP Mazembe ambayo ipo kwenye nafasi ya 10 nayo imefunika mbaya kwani inashika nafasi ya pili kwa kutwaa mataji ya Ligi ya mabingwa ikiwa imeshinda mara tano, hivyo kuongeza deni kwa Simba. Mazembe imeshinda pia mataji mawili ya Shirikisho.
MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment