ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 19, 2018

Ajali ya gari la Polisi (FFU) Yaua Polisi Wawili na Kujeruhi 9

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu pamoja na ajali za barabarani ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. Hata hivyo kwa siku ya jana kumekuwa na ajali 01 ya barabarani kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 18.01.2018 majira ya saa 16:45 jioni huko eneo la Iwambi, Kata ya Iwambi, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya kwenda Tunduma, Gari yenye namba za usajili PT 2079 Toyota Land Rover mali ya Jeshi la Polisi Kikosi cha FFU – Mbeya  ikiendeshwa na askari namba G. 3452 PC ADAM [30] Mkazi wa Iganzo ikitokea Mbeya Mjini kuelekea Mbalizi iliacha njia na kupinduka kisha kusababisha vifo kwa askari wawili ambao ni 1. H. 4335 PC MATHEW JAILOS MPOGOLE [26] na 2. H. 1215 PC PROSPER JORDAN CHALAMILA [29].

Aidha katika ajali hiyo, askari 09 walijeruhiwa ambapo kati yao majeruhi wawili wamelazwa Hospitali ya Rufaa Mbeya na majeruhi saba wametibiwa na kuruhusiwa. Waliolazwa ni 1. H. 6952 PC KELVIN MARTIN [28] Mkazi wa forest ameumia kichwani na 2. G. 3452 PC ADAM [30] Mkazi wa Iganzo, Dereva.

Aidha majeruhi wengine waliotibiwa na kuruhusiwa ni 1. H. 3929 PC LEONARD MICHAEL [26] ambaye ameumia mkono wa kushoto, 2. H. 469 PC FREDY MBANDE [28] ambaye ameumia mgongoni, 3. H. 948 PC DAVID IBRAHIM [27] ambaye amepata maumivu mwilini, 4. G. 9588 PC MARWA [29] ambaye amepata maumivu mwilini, 5. H. 1325 PC CHRISTOPHER DANIEL MSANGI [26] ambaye ameumia mbavu, 6. H. 6789 PC LUCAS ANDREA MASHALA, [24] ambaye ameumia kichwani na mbavu upande wa kulia na 7. G. 6849 PC HAMIS ALLY [32] ambaye amevunjika mkono wa kulia.

Chanzo cha ajali ni mwendokasi akijaribu kuyapita magari mengine pamoja na utelezi katika barabara. Upelelezi unaendelea. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya na majeruhi wamelazwa Hospitalini hapo. Taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kwenda nyumbani kwao Iringa zinafanyika.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha madereva kuzingatia udereva wa kujihami hasa kutokana na utelezi na kujiepusha na uendeshaji wa mwendo kasi. Aidha Kamanda MPINGA anatoa rai kwa madereva  kuzingatia sheria na kanuni zote za usalama barabarani.

        Imesainiwa na:        
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments: