ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 9, 2018

Diwani wa Chadema Iringa aeleza siri ya wenzake kujiuzulu


By Geofrey Nyang’oro, Mwananchi

Iringa. Diwani Kata ya Mivinjeni (Chadema), Frank Nyalusi ametaja sababu za madiwani wanane wa chama hicho kujiuzulu kuwa ni mgogoro uliotokana na uchaguzi wa naibu meya uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Katika uchaguzi huo Diwani wa Kata ya Gangilonga, Dadi Igogo alichaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Joseph Ryata wa Kata ya Kwakilosa ambaye alikuwa amemaliza muda wake.

“Mimi niseme tu kilichosababisha madiwani wote nane kuondoka ndani ya Chadema ni uchaguzi wa naibu meya, katika uchaguzi ule chama kidogo kiliteleza, madiwani tulikaa na kukubaliana kuwa Ryata aendelee na unaibu meya, baada ya kukubaliana watu watatu walifanya mabadiliko na kuondoa jina la Ryata na kuweka la Igogo,” amesema Nyalusi na kuongeza:

“Na hii ni matokeo ya watu kung’ang’ania madaraka chanzo cha kuondolewa kwenye nafasi yangu ya mwenyekiti wa wilaya ilikuwa ni hiyo mimi nilihoji kwa kuwa naibu meya amefanya vizuri aendelee kwa sababu vyama vya upinzani huingiziwa matatizo kipindi cha uchaguzi,” amesema.

Hata hivyo, Nyalusi ambaye amesema yeye hatajiuzulu nafasi yake ya udiwani kwa kuwa wamekaa na kukubaliana kwenye kikao ambacho wamemaliza mgogoro huo na kukubaliana kila mtu sehemu aliyokoea na kwamba dhambi waliyobaki nayo madiwani waliojiuzulu ni kukosa uvumilivu.

No comments: