Advertisements

Friday, January 12, 2018

SERIKALI KUVIPA KIPAUMBELE VIWANDA VYA NDANI VINAVYOZALISHA YA VIFAA VYA MAJI

 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akipokea maelekezo kutoka kwa Meneja Mradi wa Kiwanda cha Kahama Oil Mills, Jiten Divecha (kulia) ambacho moja ya shughuli zake ni kuzalisha vifaa vya maji kilichopo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga alipotembelea kiwandani hapo.
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akihakiki ubora wa maji yanayozalishwa na mradi wa pamoja (Joint Water Partnership Project) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na halmashauri za wilaya ya Shinyanga na Msalala kwa mkoa wa Shinyanga na Nyangh'wale kwa Mkoa wa Geita.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kakola ambacho ni miongoni mwa vijiji 13 vitakavyonufaika na mradi wa pamoja (Joint Water Partnership Project) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na halmashauri za wilaya ya Shinyanga na Msalala kwa mkoa wa Shinyanga na Nyangh'wale kwa Mkoa wa Geita.
 Baadhi ya mabomba yanayozalishwa na Kiwanda cha Kahama Oil Mills kilichopo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso amesema Serikali ya Rais Magufuli kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetoa kipaumbele kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa zinazotumika kutekeleza miradi mikubwa ya maji inayoendelea kujengwa nchini kote.
Aweso ametoa kauli hiyo mjini Kahama alipotembelea kiwanda cha Kahama Oil Mills, mkoani Shinyanga ambacho moja ya shughuli zake ni kutengeneza mabomba na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutekeleza miradi ya maji na kutoa angalizo kwamba ni lazima viwanda vya ndani vizingatie ubora wa bidhaa zao na kukidhi mahitaji halisi ya miradi yote ya maji nchini.
‘‘Hatuna sababu ya kutotumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu vya ndani, maadamu vinazingatia ubora wa bidhaa inazozalisha na kukidhi mahitaji ya nchi yetu. Serikali ya Rais Magufuli imetoa kipaumbele kwa wazalendo nchini, hivyo tumieni fursa hii na kutomuangusha,’’ alisema Aweso.
Meneja wa Kahama Oil Mills, John Zimudo kwa upande wake akizungumza wakati wa ziara hiyo anasema amefarijika sana kwa ujio wa Naibu Waziri wa Maji na Umwagilaji, na kutoa shukurani kwa Serikali ya Awamu ya Tano za kuunga mkono juhudi za wazawa katika kuinua Sekta za Viwanda nchini, huku akiahidi kutekeleza azma ya Rais Magufuli ya kujenga Tanzania ya Viwanda kwa vitendo.
Aidha, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amekagua hatua ya utekelezaji wa mradi wa maji wa pamoja (Joint Water Partnership Project) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na halmashauri za wilaya ya Shinyanga na Msalala kwa mkoa wa Shinyanga na Nyangh'wale kwa Mkoa wa Geita.
Mradi huo ukikamilika utahudumia vijiji 13 vya Mwenge, Nyugwa, Kharumwa, Mwamakiliga, Izunya, Kafita, Lushimba, Rwabakanga, Kakola namba 9, Bushingwe, Kakola, Bugarama, na Ilogi.

No comments: