Advertisements

Sunday, February 25, 2018

BITEKO AUTAKA MGODI WA KATAVI NA KAPUFI KUAJIRI WATANZANIA


aibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (katikati) wakati wa kukagua shughuli ziazofanyika kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi.
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi ili kujionea shughuli zinazoendelea mgodini hapo. Wa pili kulia ni Mbia na Makamu Mwenyekiti wa Mgodi wa Katavi & Kapufi Ltd, Sebastian Kapufi

 Moja ya eneo la mitambo kwenye mgodi wa Dhahabu wa  Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameupa Siku 14 Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo Mkoani Katavi kuhakikisha uwe umekamilisha taratibu za kuajiri Watanzania na kupunguza wafanyakazi wa kigeni kwenye nafasi ambazo Watanzania wanazimudu kama Sheria inavyoelekeza.

Alitoa agizo hili jana Tarehe 24 Februari, 2018 alipofanya ziara kwenya mgodi huo ili kujionea shughuli zinazofanyika katika mgodi huo.

Taarifa ya mgodi iliyowasilishwa kwake ilibainisha kuwa jumla ya wageni 48 wameajiriwa na huku 36 kati yao wakiwa hawana ujuzi na wanafanya shughuli ambazo Watanzania wanamudu, ikiwemo ya ulinzi.

Biteko alisema dhamira ya Serikali ni kuona Watanzania wananufaika na Sekta ya Madini kwa namna mbalimbali ikiwemo ya kujipatia ajira kwenye migodi na kwamba suala hilo la kuajiri wageni kwenye nafasi wanazomudu Watanzania halivumiliki.

Alimuagiza Mkuu wa Wilaya na Afisa Madini kuhakikisha wanalifuatilia jambo hilo na liwe limemalizika baada ya wiki mbili kuanzia Tarehe 24 Februari, 2018 na apatiwe mrejesho wake.

“Mnawafanyakazi wengi ambao wanafanya kazi ambazo Watanzania wanaziweza. Hatuwabagui lakini tunataka manufaa ya madini yabaki kwa Watanzania,” alisema Biteko.

Biteko aliiagiza Idara ya Uhamiaji Nchini kufuatilia Wafanyakazi wakigeni waliopo migodini ili kukagua kama wanavyo vibali vya kufanya kazi hapa nchini. “Mnavyotoa vibali muwe makini, ili shughuli zinazokuja kufanywa na wageni ziwe kweli Watanzania hawazimudu,” alisisitiza.

Alihimiza migodi yote nchini kuepuka kuwanyanyasa wafanyakazi sambamba na kuwataka wafanyakazi waliaoajiriwa migodini kufanya kazi kwa uaminifu ili kulijengea Taifa heshima inayokubalika.

No comments: