Advertisements

Saturday, February 24, 2018

Chadema yataka wanachama wenye majeraha kutibiwa

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Chadema wakilalamikia wanachama wake watatu kushikiliwa na polisi katika kituo cha Oysterbay wakiwa na majeraha ya risasi bila kupatiwa matibabu, Polisi Mkoa wa Kinondoni imesema hakuna mahabusu mgonjwa anayeshikiliwa bila kutibiwa.

Leo Februari 24, 2018 Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ameieleza MCL Digital kuwa wanachama hao walishambuliwa kwa risasi Februari 16, 2018.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo amesema polisi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mahabusu wagonjwa wanatibiwa katika hospitali za Serikali bila malipo yoyote.

Katika ufafanuzi wake, Mrema amebainisha kuwa wanachama hao walishambuliwa kwa risasi wakati Polisi wakiwatawanya wanachama wa chama hicho waliokuwa wakielekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kinondoni kudai barua za viapo vya mawakala wao.

Amewataja kuwa ni Isaack Ngaga, Erick John na Aida Oromi.

“John na Ngaga wao walikamatwa wakiwa majumbani mwao baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali. Hawa hawakukamatiwa kwenye vurugu,” amesema Mrema.

“Mmoja kati yao (John) alikamatwa na watu waliojifanya watumishi wa haki za binadamu na kudai kuwa wanataka kwenda kumhoji, alipokataa ndipo walitoa vitambulisho vyao vinavyoonyesha wao ni Polisi.”

Amesema hatua iliyochukuliwa hadi sasa ni kuwaelekeza wanasheria wa Chadema kufungua kesi Mahakama Kuu kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na polisi, kuwataka wawafikishe mahakamani wanachama hao.

“Tumemwelekeza mwanasheria wetu kufungua kesi ili wanachama wetu hao watatu wapelekwe mahakamani na kupatiwa matibabu,” amesema Mrema.

Amesema kuendelea kushikiliwa bila kupelekwa hospitali wakati wana majeraha ni hatari kwa maisha yao, kwa kuwa vidonda hivyo vinaoza.

“Wanakaa nao kinyume na sheria, mpaka sasa walipaswa wawe wameshawapeleka mahakamani,” amesema.

Kwa upande wake, Murilo amesema sheria ipo wazi inawaelekeza mahabusu wote wanapougua kutibiwa.

“Siyo hao mahabusu wa Chadema pekee, mahabusu yeyote anapougua hupelekwa hospitali za Serikali ambako hutibiwa bure kwa mujibu wa sheria,” amesema.

“Kama wanaolalamika wangekuwa mahabusu ningekuwa na cha kuzungumza, lakini kama wapo nje waache waendelee kusema, ninachojua hakuna mahabusu ambaye hajatibiwa.”

Mmoja wa ndugu wa Aida, Hilda Sigala amesema, “Jana nilikwenda kumtemebela ndugu yangu kituoni. Amenieleza kuwa mpaka sasa hajapelekwa hospitali na wanampaka dawa tu ya kukausha kidonda wakati ana jeraha la risasi. Yupo kituoni tangu Februari 16.”

No comments: