Advertisements

Saturday, February 10, 2018

KESI MAUAJI YA BILIONEA ERASTO MSUYA-Dada wa marehemu aangua kilio kortini

Ndugu wa watuhumiwa wa Kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya wakiwa katika Mahakama Kuu kanda ya Moshi ,kabla ya kuanza kesi kuskilizwa. Picha na Dionis Nyato

By Daniel Mjema na Fina Lyimo mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Antuja Msuya ambaye ni dada wa mfanyabiashara tajiri, marehemu Erasto Msuya, jana aliangua kilio mahakamani baada ya kuona bunduki ya kivita aina ya SMG inayodaiwa kutumika kumuua kaka yake.
Hayo yalijitokeza wakati shahidi wa 17 wa upande wa mashtaka, mrakibu wa polisi (SP), Vincent Lymo alipokuwa akitoa ushahidi wake na kuitambua bunduki hiyo yenye namba 1952 KJ 10520.
Mbele ya Jaji Salma Maghimbi anaysikiliza kesi hiyo, Antuja alianza kububujikwa machozi saa 5:35 asubuhi, wakati shahidi huyo alipokuwa akiitoa bunduki hiyo kutoka mfuko wa sandarusi.
Kwanza alianza kububujikwa na machozi huku akijifuta kwa leso, lakini kadri bunduki hiyo ilivyokuwa ikitolewa na shahidi kutoa maelezo huku akiijaribu, Antuja alishindwa kujizuia.
Dakika tano baadaye alinyanyuka na kutoka nje ya chumba cha wazi cha mahakama, lakini alipofika tu nje ya chumba hicho, alianza kulia kwa sauti kubwa na kutaka kuathiri shughuli za mahakama.
Polisi mwenye cheo cha inspekta anayesimamia shughuli za polisi ndani ya mahakama, alimfuata mwanamke huyo na kumsihi aondoka katika eneo hilo na kwenda kulilia mbali na eneo hilo.
Hata hivyo, yaliibuka mabishano makali ya kisheria wakati Lyimo ambaye mwaka 2013 alikuwa mkuu wa upelelezi (OC-CID) Wilaya ya Siha, alipotaka kuitoa bunduki hiyo kama kielelezo.
Akitoa ushahidi wake, Lyimo alieleza kuwa Septemba 11, 2013 akiwa ofisini kwake wilayani Siha, alipigiwa simu na mkuu wa upelelezi mkoa (RCO) wa Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi.
“Aliniuliza kama namfahamu Said Mohamed maarufu Mnubi anayeishi Lang’ata. Nilipomwambia namfahamu aliniambia nimtafute nimpeleke ofisini kwake kwani kuna kazi maalumu.
“Nilitafuta namba ya huyo mtu na nilipoipata nilimpigia simu akaniambia yuko maeneo ya Kibosho Road. Nilimwambia anisubiri hapo. Nilimfuata na kwenda naye ofisini kwa RCO.
“Tukiwa ofisini RCO alimhoji kama ana ndugu yake anaitwa Sadick Jabir (mshtakiwa wa sita) ambaye amekamatiwa Tabora, kwamba kuna vitu vyake yeye (Said) anajua vilipo,” alieleza.
Shahidi huyo alieleza kuwa, vitu hivyo ni pikipiki iliyokuwa imehifadhiwa katika mji wa Bomang’ombe na mfuko wa sandarusi unaodaiwa kuwa na bunduki hiyo ya SMG.
“Said alimjibu RCO kuwa anajua kuhusu pikipiki na anajua ilipo ila akasema kuna mzigo aliambiwa na kaka yake (mshtakiwa) kuwa imefichwa kwenye tindiga njia ya kuelekea Boloti,” alidai shahidi huyo na kuongeza:
“Huko Tabora, mshtakiwa huyo wa sita anadaiwa kuwaeleza polisi kuwa bunduki hiyo ilikuwa ni mali yake na kijana anayeitwa Karim. Hata hivyo, hakueleza kama ni Karim Kihundwa mshtakiwa wa tano.
“Said alihiyari kutupeleka hadi eneo ilipokuwa imefichwa hiyo bunduki lakini akasema itahitajika watu wengi wa kuitafuta kwa sababu eneo hilo ni pori. Tulifika na RCO akaagiza watafutwe watu zaid.”
Akiendelea kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alidai agizo hilo la RCO lilitekelezwa na watu zaidi ya 20 walipatikana. “Tulijipanga tukipishana umbali wa kama hatua nne kutoka kwa mtu,” alidai..
Shahidi huyo alidai kazi hiyo iliwachukua nusu saa na mzee mmoja aliyemtaja kuwa ni Joseph Hamis Mushi, alipaza sauti na kuwajulisha watafutaji kuwa ameona mfuko wa sandarusi.
“Mimi ndiye nilikuwa karibu yake kwa hiyo nilikwenda na kuuchukua huo mfuko. Nilipoufungua nilikuta bunduki ya SMG. Niliikagua na kuijaribu kama inafanya kazi nikakuta inafanya,” alieleza mahakama.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kuijaribu bunduki hiyo ambayo inaonekana ni ya kikosi cha jeshi na kusoma namba zake ambazo ni 1952 KJ, aliikabidhi kwa RCO wakati huo, Ng’anzi.
Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee bunduki hiyo na mfuko huo wa sandarusi kama kielelezo cha kesi hiyo, lakini jopo la mawakili watano wa utetezi likapinga vikali ombi hilo.
Akiwasilicha hoja za kupinga vielelezo hivyo kwa niaba ya wenzake, wakili Majura Magafu alidai bunduki hiyo haikuwa sehemu ya vielelezo vilivyotajwa wakati kesi ikihamishiwa Mahakama Kuu.
Aliiambia mahakama kuwa mchakato wa kuihamishia kesi mahakama kuu (committal proceedings), uliofanyika Juni 10, 2014 mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Munga Sabuni, bunduki hiyo haikuelezewa.
“Vielelezo vilivyozungumziwa siku hiyo vilikuwa 17 na documentary evidence (vielelezo vya nyaraka) 17. Hapakuwa na maelezo kutoka upande wa mashtaka kuwa watawasilisha kielelezo halisi,” alidai.
Wakili Magafu aliendelea kuwa kifungu namba 246(2) (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinasisitiza umuhimu wa kuorodhesha vielelezo wakati wa mchakato wa kuihamisha kesi ya mauaji.
Alidai kuwa wakati wa usikilizwaji wa awali wakati kesi hiyo ilipofikishwa mara ya kwanza mahakama kuu, kulikuwa na jaribio la kuitoa bunduki hiyo kama kielelezo lakini mawakili wa utetezi walipinga.
“Defence (mawakili wa utetezi) wakakataa wakasema vitolewe wakati wa usikilizaji wa kesi. Waliomba ku tender (kutoa) SMG na pikipiki lakini hakuna sehemu inasema watatoa mfuko wa sandarusi,” alieleza.
Magafu alidai hakuna ubishi kuwa katika maelezo yake, Lyimo anazungumzia pikipiki, bunduki na sandarusi lakini hiyo haitoshi kwa kuwa walitakiwa waorodheshe vielelezo vyao halisi.
Pia, wakili huyo anayesadiana na Aloyce Qamara, Emmanuel Safari, Hudson Ndusyepo na John Lundu, alidai shahidi huyo hana sifa (competence) ya kuwa mtu wa kutoa vielelezo hivyo mahakamani.
Aliendelea kuwa mtu sahihi wa kuvitoa mahakamani alipaswa awe mzee Joseph Hamis Mushi, siyo shahidi kwa vile hata hiyo jana, haijaelezwa kielelezo hicho kilifikaje mikononi mwake.
Pia, alidai kuwa sababu nyingine ya kupinga ni katika ushahidi wa Lyimo hajaeleza wala kutoa fomu PF 16 ambayo ni rejista ya vielelezo kuonyesha mnyororo wa makabidhiano.
Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali mwandamizi, Abdallah Chavula alidai kifungu namba 246 (2)(6) walichokiegemea mawakili wa utetezi, kinazungumzia ushahidi wa nyaraka siyo wa vitu halisi.
“Vifungu hivyo vinazungumzia documentary evidence (ushahidi wa nyaraka) na hakijasema kwamba hicho kifungu kinakuwa extended (kinajiongeza) hadi kwenye physical evidence (ushahidi halisi),” alieleza.
Kuhusu Lyimo kuwa siyo shahidi anayestahili kutoa vielelezo hivyo, alidai kuwa ni shahidi sahihi kwa vile kwanza ana ufahamu wa kielelezo chenyewe, ndiye aliyekiokota, kukikagua na kukijaribu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo, Jaji Maghimbi anayeisikiliza atakapotoa uamuzi wake iwapo bunduki hiyo na mfuko huo wa sandarusi vipokelewe kama kielelezo au la.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kwa kutumia bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi inawakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed na Ally Mussa.
Bilionea Msuya ni nani?
Erasto Msuya alizaliwa miaka 43 iliyopita (1970) akiwa mtoto wa kwanza wa mzee Kikaango Msuya na miongoni mwa wafanyabiashara waliomudu vyema biashara ya madini ya Tanzanite.
Ni kutokana na biashara hiyo ya Madini, Msuya aliweza kumiliki mali nyingi yakiwamo magari ya kifahari na vikiwamo vitega uchumi mbalimbali katika Jiji la Arusha na mji wa Mererani.
Katika mji wa Mererani katika wilaya ya Simanjiro, Msuya ndiye aliyekuwa mfanyabiashara wa kwanza kumiliki jengo la ghorofa katika mji wa Mererani karibu na stendi ya mabasi.
Si hivyo tu, lakini Bilionea Msuya alikuwa akimiliki hoteli za kitalii zenye hadhi ya nyota tano za SG Resort na Mezza Luna zilizopo katika jiji la Arusha ambalo ni maarufu kwa biashara ya utalii.
Pia Alikuwa akimiliki magari ya kifahari likiwamo gari aina ya Range Rover lililokuwa toleo jipya wakati akiuawa, likiwa na thamani ya Dola 250,000 za Marekani sawa na Sh400 milioni wakati huo.

No comments: