ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 18, 2018

SERIKALI KUMFIKISHA MAHAKAMANI MKANDARASI WA JENGO JIPYA LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE SONGWE

Muonekano wa jengo jipya la abiria ambalo halijamalizika ujenzi wake la uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya kama lilivyokutwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati wa ziara yake uwanjani hapo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akipita kwenye eneo la uwanja wa ndege wa Mbeya ambao wananchi wamepimiwa viwanja 75 vya makazi kimakosa ambapo Serikali inaurejesha kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, mmiliki halali wa eneo hilo ili uendelezwe. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Bwana William Paul Ntinika
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzina Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akimhoji Mhandisi Magesa Mwita wa TANROADS, Mbeya kuhusu taarifa anayoitoa kwake ya maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya wakati wa ziara yake uwanjani hapo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzina Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya wakati wa ziara yake uwanjani hapo

Na Wuum, SONGWE
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye ameielekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kumfikisha mahakamani mkandarasi anayejenga jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Songwe lenye uwezo wa kuchukua abiria 1,500,000 kwa mwaka.
Mhandisi Nditiye ametoa maelekezo hayo kwa TAA wakati wa ziara yake uwanjani hapo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja huo. “Naielekeza TAA kuchukua hatua za kisheria kwa kampuni hii ya DB Shapriya na kumpeleka mahakamani mkandarasi huyu kwa kuwa mkataba wa miezi minane umechukua miaka mitano na Serikali imeshamlipa fedha zote tangu mwaka 2015”, amefafanua Mhandisi Nditiye.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli haiko tayari kumvumilia mkandarasi yeyote anayetumia vibaya pesa ya Serikali ya wananchi walipa kodi, hivyo mkandarasi huyu ataitema fedha hii.
Mhandisi Nditiye ameongeza kuwa Serikali itamshitaki mkandarasi huyu kwenye Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Serikali haiko tayari kuendelea kufanya kazi na wakandarasi wa namna hii. Aidha, amewahakikishia wananchi watanzania kuwa jengo hilo litakamilika na Serikali itatafuta mkandarasi mwingine.
Mhandisi Nditiye ameitaka TAA kuanzia tarehe 31 Januari mwaka huu ambapo ilipewa maelekezo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ianze kuikata fidia ya uchelewashaji wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo mkandarasi huyo.
Naye Mhandisi Mshauri wa kampuni ya kiuhandisi ya UNETEC kutoka Dubai Mhandisi Silanda Dustan amesema kuwa mkandarasi hajafikia kiwango kinachotakiwa cha kujenga jengo hilo la abiria ambapo wananchi wanakosa huduma na Serikali inakosa mapato.
Serikali iliingia mkataba wa kazi ya kujenga jengo jipya la abiria la uwanja huo na mkandarasi DB Shapriya wa Tanzania wa gharama ya shilingi bilioni kumi na moja. Mkataba huo ulisainiwa mwezi Februari mwaka 2013 na kazi ya kujenga jengo hilo jipya la abiria ilitarajiwa kukamilika ndani ya miezi minane hadi mwezi Oktoba mwaka 2013.
Akiwa uwanjani hapo, Mhandisi Nditiye ametembelea uwanja huo ili kukagua na kujiridhisha kuhusu suala la ukosefu wa taa za kuongoza ndege ambapo jambo hilo limezungumzwa kwenye vikao baina ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu. Amebaini kuwa uwanja huo hauna taa na hauwezi kufanya kazi saa 24 ambapo lengo la Serikali ni kuufanya uwanja huo kuwa wa kimataifa na kwa sasa unahudumia abiria wa nchi za jirani za Malawi, Zambia na RDC Congo.
Meneja wa Uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya Bwana Hamisi Amiri amesema kuwa tayari mkandarasi wa kampuni ya GECI Ispanola amepatikana kwa ajili ya kuweka taa za kuongoza ndege kwa gharama ya shilingi bilioni 4.7 ambapo inajumuisha taa za barabara ya kuruka na kutua ndege na taa za barabara. Ameongeza kuwa uwanja wa ndege wa Songwe una uwezo sawa na uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere wa Dar es Salaam wa kutua ndege kubwa ambapo kiwanja kina ukubwa wa eneo la hekari 1,800 na barabara ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa mita 3333 na upana wa mita 45.
Katika hatua nyingine Mhandisi Nditiye ametembelea uwanja wa ndege wa Mbeya wenye ukubwa wa hekari 179 uliovamiwa na wananchi ambapo maafisa ardhi wasio waaminifu wamepima viwanja 75 vya makazi na kuwapatia wananchi, na amelaani kitendo hicho na Serikali itawachukulia hatua maafisa waliohusika. Pia amewaelekeza TAA kuwekeza kwenye uwanja huo kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kuwa Serikali imefuta hati za viwanja hivyo na itaipatia TAA hati miliki ya eneo lake. Pia, amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Amos Makalla kwa kufuatilia eneo hilo na kuzuia wananchi kuliendeleza.
Naye Katibu Tawala Msaidizi wa Miundombinu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Jeremia Minja amefafanua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Amosi Makalla amesimamisha zoezi la wananchi kumiliki viwanja vya makazi na ameielekeza TAA kujipanga kuendeleza eneo hilo.
Meneja wa uwanja wa ndege wa Songwe, Mbeya Bwana Hamisi Amiri amesema kuwa TAA itapima eneo hilo haraka mara baada ya kupata hati miliki kutoka kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

No comments: