ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 27, 2018

SERIKALI YAOMBWA KUONDOA KODI ZA PEMBEJEO ZA KILIMO

 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Endasaboghechani wakimpokea Mbunge wa jimbo la Hanang, Mkoani Manyara, Dk. Mary Nagu alipowasili katika Kijiji hicho kwa ajili ya kufanya ziara ya kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge wa jimbo hilo.
 Mbunge wa jimbo la Hanang, Mkoani Manyara, Dk. Mary Nagu akikagua majengo ya kituo cha afya kinachotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kijiji hicho pamoja na vijiji jirani. 
 Kikundi cha ngoma cha Upendo kinachotumbuiza wananchi kwa ngoma za kabila la wanyiramba wakati wa ziara ya Mbunge wa jimbo la Hanang, Dk. Mary Nagu
 Bibi Terecia Michaeli akiwa katika mkutano wa Mbunge wa jimbo la Hanang, Dk. Mary Nagu ambapo pamoja na mambo mengine bibi huyo alitaka kufahamishwa sababu zilizochangia wazee wasiokuwa na uwezo katika Kijiji hicho kutoingizwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini(TASAF)(Picha zote Na Jumbe Ismailly)

Na. Jumbe Ismailly 
SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kuondoa kodi kwenye pembejeo za kilimo na mifugo ili kuwasaidia wakulima kuwa na uwezo wa kulima na kufuga kwa njia za kisasa na kuwawezesha kujiongezea kipato katika familia na taifa kwa ujumla.
Ombi hilo limetolewa na Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,Dk.Mary Nagu kwenye vijiji vya Kidagharbu na Endasaboghechani alipokuwa akiongea na wananchi wa vijiji hivyo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuwashukuru kwa kumchagua kwa kura nyingi kuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Namuomba na nitazidi kumuomba rais Magufuli na serikali mheshimiwa wangu kwamba ondoeni kodi kwenye kilimo ili watu walime,na nikisema kilimo ni pamoja na mifugo”alisisitiza Dk.Nagu.
Aidha alifafanua mbunge huyo kwamba endapo wakulima watalipa kwa nguvu zote na mpaka watakapoenda sokoni kuuza na kwamba fedha watakazopata watanunua bati za kujenga nyumba zao bora na za kisasa zaidi.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wakulima na wafugaji watalipa kodi za serikali watakaponunua bati,saruji na sukari na kuonya kwamba endapo wakulima hao hawakufanikiwa kupata fedha kwenye kilimo,vifaa vyote hivyo havitaweza kununuliwa na hivyo kuikosesha serikali kodi yake.
Hata hivyo Dk.Nagu alisisitiza kwamba pamoja na serikali kuondoa kodi kwenye mbegu lakini bado bei za mbegu zipo juu,jambo ambalo linadhihirisha kwamba bado kuna watu wa kati wanaonufaika kupitia kuuzwa kwa mbegu hizo kwa bei ya juu.
Hata hivyo baadhi ya wananchi walitaka kupatiwa ufafanuzi wa baadhi ya mambo ambapo kwa upande wake mkazi wa Kijiji cha Endasaboghechani,Terecia Michaeli alitaka kufahamu sababu zilizochangia wazee wasiokuwa na uwezo kutoingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini unaosimamiwa na TASAF.

Akijibu hoja za wanannchi,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Benedicto Ngaiza licha ya kukiri kwamba bado kuna maeneo ya vijiji vingine kutoingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini,lakini hata hivyo aliwahakikishia wananchi hao kwamba vijiji vilivyobakia vitaingizwa kwenye awamu nyingine ya mpango huo.

No comments: