Mkazi wa Kata ya Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, Julius Benjamin akimweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa (mbele) kuhusu changamoto ya miundombinu ya barabara katika eneo hilo jana Jumamosi (Februari 17, 2018) wakati wa ziara ya Naibu Waziri kukagua miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Tanga.
Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
WANANCHI wa Kata ya Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwajengea barabara ya kiwango cha lami katika Kata hiyo kwa kuwa eneo hilo kwa sasa limekuwa tegemeo kubwa katika kutoa huduma za kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Tanga.
Wakiwasilisha malalamiko yao mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa jana Jumamosi Februari 16, 2018 aliyekuwa katika ziara ya kukagua miradi ya barabara katika Mkoa wa Tanga, wananchi hao walisema eneo hilo limekuwa vigumu kupitika wakati wa mvua za masika na hivyo kusababisha kero kwa wananchi.
Mmoja wa wananchi hao, Bw. Julius Benjamin alisema tangu kuanzishwa kwa mji huo mwaka 2004, kumekuwepo na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, pamoja na eneo hilo kuwa kiunganishi cha Wilaya za Mkinga, Korogwe na Muheza Mkoani humo.
“Hata ukitazama katika ramani utaona kuwa eneo la marimba lipo tangu mwaka 1919 na lilikuwa maarufu sana katika shughuli za uchimbaji wa madini, lakini pamoja na kuwa ni eneo la kihistoria miundombinu ya barabara katika eneo letu limekuwa ni tatizo kubwa hususani kipindi cha mvua za masika” alisema Julius.
Aidha aliongeza kuwa pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa na wananchi wa eneo hilo kwa ajili ya kufikisha kilio chao, eneo hilo bado limeendelea kuwa na tatizo la barabara, hivyo ujio wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika Kata hiyo unatarajia kulipatia ufumbuzi jambo hilo.
Naye Bw. Juma Ahmed alisema pamoja na eneo hilo kuwa tegemeo la kiuchumi katika Mkoa wa Tanga, kwa kipindi kirefu Serikali imeshindwa kutengeneza miundombinu ya uhakika wa barabara ambazo zitawawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Anaongeza kuwa barabara hiyo pia imekuwa ni nyembamba pamoja na kuwa na pilikapilika mbalimbali za huduma za kijamii na kiuchumi, hivyo kuiomba Serikali kuitazama kwa jicho la tatu eneo hilo kwa kuwapatia miundombinu ya uhakika nma hivyo kumaliza kilio cha muda mrefu kwa wananchi hao.
Akijibu hoja za wananchi hao, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa alisema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya uhakika katika Mkoa wa Tanga ikiwemo ujenzi wa barabara hatua inayolenga kuinua uchumi wa Mkoa na kipato cha wananchi kwa ujumla wake.
“Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi usiku na mchana katika kumaliza changamoto mbalimbali za wananchi wake ikiwemob uimarishaji wa miundombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi ikiwemo barabara, hivyo tumejipanga kuwatumikia” alisema Kwandikwa.
Aliongeza Serikali ipo mbioni kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya Maramba ikiwemo kuanza zoezi la upembuzi yakinifu na kuanza michoro ya eneo hilo kwa ajili ya kutambua mahitaji yake na baadaye kuanza mara moja ujenzi wake.
Kwa mujibu wa Kwandikwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaweza kuharakisha shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo uzalishaji wa mazao na usafirishaji wa pembejeo za kilimo na hivyo kufungua fursa kwa wakazi wa eneo hilo kujiimarisha kiuchumi.
No comments:
Post a Comment