Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ya Nchi Mhe.Dr. Mwigulu Lameck Nchemba akiwasili kwenye viwanja vya Shujaa Morogoro kwenye sherehe za uzinduzi wa Zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu kwa mkoa huo. Hapa anasalimiana na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Paschal Kihanga.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Dr. Kebwe Steven Kebwe akisoma taarifa kuhusu mkakati wa mkoa kuwasajili wananchi zaidi ya 960,000 wakati wa sherehe za Uzinduzi wa zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa.
Mbunge wa Morogoro Mjini Mhe. Aziz Abood akitoa salamu kwa wananchi waliofurika kushuhudia sherehe za Uzinduzi wa zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Dr. Mwigulu Lameck Nchemba akihutubia wananchi wakati wa Uzinduzi wa zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu wenye lengo la Kutoa Vitambulisho vya Taifa Morogoro.
Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizindua shughuli za Usajili na Utambuzi wa Watu katika Mkoa wa Morogoro Jumamosi katika viwanja vya Shujaa mkoani humo na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA ndugu Andrew Massawe akisoma taarifa ya zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu kwa mikoa 19 inayoendelea na Usajili; amesema mkoa wa Morogoro unakusudiwa kusajiliwa zaidi ya wananchi 960,000 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Zoezi ambalo limepangwa kukamilika kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili,2018.
“ Mkoa wa Morogoro zoezi litahusisha Wilaya zote isipokuwa Kilombero ambayo ilikuwa Wilaya ya kwanza ya mfan kufanyiwa usajili mwaka 2012 na hivyo idadi kubwa ya wananchi wake tayari wana Vitambulisho vya Taifa na kwasasa wanaosajiliwa ni wale wanaotimiza umri wa miaka 18 na wanaohamia “ asisisitiza
Aidha ndugu Massawe amemweleza Mhe. Waziri mbali na Usajili Mamlaka kwa kushirikiana na wadau wengine imeanza matumizi ya Vitambulisho vya Taifa ikiwemo Usajili wa Makampuni unaofanywa na Brella ambao kwa sasa unataka kila anayesajili Kampuni kuwa na Kitambulisho cha Taifa. Huduma nyingine ambazo kwa sasa huwezi kuzipata bila kuwa na Kitambulisho cha Taifa ni upatikanaji wa Hati za kusafiria(Passport), Usajili wa namba za simu na huduma nyingine za kifedha n.k
Katika hotuba yake Mhe. Waziri amekemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji na Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji kudai posho au kuhusisha michango na tozo mbalimbali wakati wa kuwasajili wananchi wakati zoezi hilo ni bure. Amesisitiza Mamlaka zote za Serikali kuhakikisha zinasisimia na kutoa ushirikiano kwa NIDA kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanasajiliwa kwa wakati wakiwemo Wageni na Wakimbizi kwani shughuli ya usajili kwa sasa inahusisha makundi yote. Pindi wakati utakapofika kwa wale wote ambao watakuwa hawakusajiliwa watakuwa na cha kujieleza kwanini hawakusajiliwa Vitambulisho vya Taifa wakati Serikali imewekeza fedha nyingi kukamilisha zoezi hili.
Amesisitiza Usajili Vitambulisho vya Taifa si hiyari ni wajibu wa kila Raia, Mgeni na Mkumbizi kusajiliwa kwa kufuata taratibu, sharia na kanuni za Usajili zinazosimamiwa wakati wa utekelezaji wa Usajili.
“ Kama mnavyofahamu Serikali ya Awamu ya Tano chini Mhe. Dr. John Pombe Magufuli ina vipaumbele vingi na mahitaji kwa wananchi ni mengi. Sasa Rais ameacha mambo mengine akaamua kuwekeza kwenye Vitambulisho vya Taifa mradi unaoigharimu Serikali fedha nyingi sana; sasa ole wao ambao hawatasajiliwa kwa visingizio visivyokuwa na msingi” alisisitiza
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Dr. Kebwe Steven Kebwe amewataka wananchi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kwenye Usajili wa Vitambulisho vya Taifa unaoendelea maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kusisitiza hatowafumbia macho wale wote watakao husisha zoezi hilo na itikadi za vyama au dini, au kudai rushwa kuwahudumia wananchi pindi wanapojitokeza kwenye vituo vya kusajiliwa.
Zoezi la Usajili wanachi Vitambulisho vya Taifa linakusudiwa kumalizika mwezi Desemba mwaka huu kwa wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kuwa wamesajiliwa na kupata namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) wakati hatua za Uzalishaji zikiendelea sambamba na kuvigawa kwa wananchi.
Waziri Mwigulu akiwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Ndugu Andrew Massawe kukagua mashine zitakazotumika kukusanya taarifa za wananchi wakati wa uzindizi wa zoezi la Usajili kwa mkoa wa Morogoro.
Mhe. Waziri (Katikati) akizindua rasmi kuanza kwa Usajili Vitambulisho vya Taifa mkoani Morogoro. Wengine ni Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dr. Kebwe Steven Kebwe (Wa kwanza kulia), Mbunge wa Morogoro Mjini Mhe. Aziz Abood (Wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Ndugu Andrew Massawe (watatu kulia), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kiyanga ( wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo (wa kwanza kushoto).
Mhe Waziri wa Mambo ya Nchi pamoja na viongozi wengine wakishuhudia mmoja wa wananchi Bi. Rehema Abdallah akisajiliwa kwa mara ya kwanza na taarifa zake kuingizwa moja kwa moja kwenye mfumo wa NIDA wakati wa sherehe za Uzinduzi Vitambulisho vya Taifa mkoani Morogoro.
Pamoja na kuzindua kuanza kwa zoezi la Usajili Vitambulisho mkoani Morogoro Waziri Mwigulu pia alizindua kuanza kutolewa Vitambulisho kwa wananchi ambao wamekamilisha taratibu za Usajili. Hapa anamkabidhi Bi. Jackline Kayombo kitambulisho chake.
No comments:
Post a Comment