Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi akibadilishana mawazo na Jaji Mkuu wa Gambia Mhe. Hassan Bubacar Jallow, leo Ofisi kwa Mwanasheria Mkuu. Jaji Mkuu yupo hapa nchini kwa ziara ya kikazi yenye madhumuni ya kujifunza uboreshaji wa sekta ya sheria na utoaji haki hapa nchini. Baadhi ya mambo waliyobadilishana mawazo ni pamoja na uwezeshwaji kwa wanasheria wa Serikali na watumishi wengine katika sekta ya sheria kimaslahi na kimafunzo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiagana na Mgeni wake Jaji Mkuu wa Gambia Mhe. Hassan Bubacar Jallow mara baada ya mazungumzo yao. Jaji Mkuu Jallow alisoma sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1970-1973) na pia amewaji kuwa Mwendesha Mashtaka wa iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) (2003-2015).
Mwanasheria Mkuu Dk. Adelardus Kilangi akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe Wilbroad Slaa walipokutana nje ya Jengo ambalo lina Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki . Mwanasheria Mkuu alikuwa akimsubiri kumpokea mgeni wake Jaji Mkuu wa Gambia Mhe. Hassan Jallow ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
Anwani ya Simu “LEGAL” Dar es Salaam
Simu: +255-2118178/82 20 Barabara ya Kivukoni
Fax No: +255-2113236 11492 Dar es Salaam
S.L.P 9050
Tanzania.
JAJI MKUU WA GAMBIA AMTEMBELEA MWANASHERIA MKUU.
Na Mwandishi Maalum
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, leo (Alhamisi) amekutana na kuwa na mazungumzo na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Gambia Mhe. Hassan Bubacar Jallow.
Jaji Mkuu wa Gambia, yupo hapa nchini kwa ziara ya kikazi ya kujifunza na kujipatia uzoefu kuhusu mfumo wa utoaji haki hapa nchini pamoja na maboresho mbalimbali yakiwamo ya maslahi ya watumishi yanayoendelea katika Mahakama ya Tanzania na Taasisi nyingine za Sheria na utoaji haki.
Jaji Mkuu Jallow amemueleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi kwamba, Gambia, baada ya mabadiliko ya Serikali yaliyofanyika mwaka jana nchini humo, ipo katika mchakato wa kuifanyia mabadiliko na maboresho sekta ya sheria nchini humo.
"Nimekuja kwa ziara ya kikazi kwa madhumuni ya kujifunza kutoka Tanzania namna gani na sisi (Gambia) tutakavyoweza kuboresha na kuifanyia mageuzi makubwa sekta yetu ya Sheria na mfumo mzima wa utoaji wa haki".
Akabainisha kwamba, anafahamu, namna gani Mahakama ya Tanzania imeweza, kwa kushirikiana na Serikali na Wadau wa Maendeleleo hususani Benki ya Dunia kufanya mageuzi na maboresha makubwa katika mfumo wa utoaji haki.
"Ningependa kujifunza mbinu ambazo Mahakama iliweza kuzitumia kuivutia Benki ya Dunia hata ikawa mdau wake muhimu katika maboresha yanayoendelea hivi sasa. Na pia nitumie fursa hii kubadilishana mawazo pamona na wewe Mwanasheria Mkuu na nikupongeze kwa kuteuliwa kwako." akaeleza Jaji Mkuu.
Pamoja na kumtembelea Mwanasheria Mkuu wa Serikali, miongoni mwa sehemu anazotarajiwa kutembelea kama sehemu ya kujipatia uzoefu ni Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
" Ninakwenda pia Lushoto na pamoja na mambo mengine ninataka kuangalia uwezekano wa kuanzisha ushirikiano na Chuo hicho kwa kuwaleta watu wetu na pia kuwaalika wataalamu kutoka Chuo hicho kuja nchini Gambia". amesisiza Jaji Mkuu Jallow.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu ameunga mkono wazo la Jaji Mkuu la kuanzisha uhusiano wa karibu na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kile alichosema ni moja ya Taasisi muhimu sana katika utoaji wa mafunzo.
Akabainisha kuwa hata Ofisi ya Mwanasheria Mkuu nayo inaangalia namna bora zaidi ya kukitumia Chuo katika kuwajenga uwezo na kuwapiga msasa wafanyakazi wa Ofisi yake.
Kuhusu maslahi na mazingira bora ya kufanyia kazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni eneo ambalo linatakiwa kuangaliwa na kufanyiwa kazi.
"Maslahi ya wafanyakazi katika sekta ya utoaji haki ni muhimu sana, na hasa ukizingatia kwa mfano katika Ofisi yangu , wanafanya kazi kubwa, nzuri, kwa uadilifu na uzalendo wa hali ya juu sana. Kuna haja na umuhimu wakuangalia pia maslahi yao ili siyo tu kuwapa motisha ya kutekeleza majukumu yao vizuri zaidi lakini pia kuwafanya wapende kubaki na kufanya kazi serikalini. akaeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Dk. Kilangi amemshukuru Jaji Mkuu wa Gambia kwa kuitembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na kubadilishana uzoefu na kwamba wakati wowote Ofisi hiyo itakuwa tayari kushirikiana na Gambia kupitia sekta ya sheria na utoaji haki.
Jaji Mkuu Hassan Jallow pia si mgeni sana kwa Tanzania kwa sababu shahada yake ya kwanza ya Sheria aliipata katika Chuo Kikuu cha Dar Es s Salaam ( 1973) na pia amewahi kuwa Mwendesha Mashtaka wa iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) (2003-2015)
No comments:
Post a Comment